Zab. 29 Swahili Union Version (SUV)

Sauti ya Mungu katika Dhoruba

1. Mpeni BWANA, enyi wana wa Mungu,Mpeni BWANA utukufu na nguvu;

2. Mpeni BWANA utukufu wa jina lake;Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu.

3. Sauti ya BWANA i juu ya maji;Mungu wa utukufu alipiga radi;BWANA yu juu ya maji mengi.

4. Sauti ya BWANA ina nguvu;Sauti ya BWANA ina adhama;

5. Sauti ya BWANA yaivunja mierezi;Naam, BWANA aivunja-vunja mierezi ya Lebanoni;

6. Airusha-rusha kama ndama wa ng’ombe;Lebanoni na Sirioni kama mwana-nyati.

7. Sauti ya BWANA yaipasua miali ya moto;

8. Sauti ya BWANA yalitetemesha jangwa;BWANA alitetemesha jangwa la Kadeshi.

9. Sauti ya BWANA yawazalisha ayala,Na kuifichua misitu;Na ndani ya hekalu lakeWanasema wote, Utukufu.

10. BWANA aliketi juu ya Gharika;Naam, BWANA ameketi hali ya mfalme milele.