Zab. 75 Swahili Union Version (SUV)

Shukrani kwa Wema Aliotenda Mungu

1. Ee Mungu, twakushukuru.Twakushukuru kwa kuwa Jina lako li karibu;Watu huyasimulia matendo yako ya ajabu.

2. Nitakapoufikia wakati ulioamriwa,Mimi nitahukumu hukumu za haki.

3. Ingawa dunia na wote wakaao humo wataharuki,Mimi mwenyewe nimezisimamisha nguzo zake.

4. Naliwaambia waliojivuna, Msijivune;Na wasio haki, Msiiinue pembe.

5. Msiiinue pembe yenu juu,Wala msinene kwa shingo ya kiburi.

6. Maana siko mashariki wala magharibi,Wala nyikani itokako heshima.

7. Bali Mungu ndiye ahukumuye;Humdhili huyu na kumwinua huyu.

8. Maana mkononi mwa BWANA mna kikombe,Na mvinyo yake inatoka povu;Kumejaa machanganyiko;Naye huyamimina.Na sira zake wasio haki wa duniaWatazifyonza na kuzinywa.

9. Bali mimi nitatangaza matendo yako milele,Nitamwimbia Mungu wa Yakobo.