Isa. 60:6-17 Swahili Union Version (SUV)

6. Wingi wa ngamia utakufunika,Ngamia vijana wa Midiani na Efa;Wote watakuja kutoka Sheba;Wataleta dhahabu na uvumba;Na kuzitangaza sifa za BWANA.

7. Makundi yote ya Kedari yatakusanyika kwako,Kondoo waume wa Nebayothi watakutumikia;Watapanda juu ya madhabahu yangu kwa kibali,Nami nitaitukuza nyumba ya utukufu wangu.

8. Ni nani hawa warukao kama wingu,Na kama njiwa waendao madirishani kwao?

9. Hakika yake visiwa vitaningojea,Na merikebu za Tarshishi kwanza,Ili kuleta wana wako kutoka mbali,Na fedha yao na dhahabu yao pamoja nao,Kwa ajili ya jina la BWANA, Mungu wako,Kwa ajili yake Mtakatifu wa Israeli,Kwa kuwa amekutukuza wewe.

10. Na wageni watajenga kuta zako,Na wafalme wao watakuhudumu;Maana katika ghadhabu yangu nalikupiga,Lakini katika upendeleo wangu nimekurehemu.

11. Malango yako nayo yatakuwa wazi daima;Hayatafungwa mchana wala usiku;Ili watu wapate kukuletea utajiri wa mataifa,Na wafalme wao wakiongozwa pamoja nao.

12. Kwa maana kila taifa na ufalme wa watuWasiotaka kukutumikia wataangamia;Naam, mataifa hayo wataharibiwa kabisa.

13. Utukufu wa Lebanoni utakujia wewe,Mberoshi na mtidhari na mteashuri pamoja;Ili kupapamba mahali pangu patakatifu,Nami nitapatukuza mahali pa miguu yangu.

14. Na wana wa watu wale waliokutesaWatakuja kwako na kukuinamia;Nao wote waliokudharauWatajiinamisha hata nyayo za miguu yako;Nao watakuita, Mji wa BWANA,Sayuni wa Mtakatifu wa Israeli.

15. Na kwa kuwa umeachwa na kuchukiwa,Hata ikawa hapana mtu aliyepita ndani yako,Nitakufanya kuwa fahari ya milele,Furaha ya vizazi vingi.

16. Utanyonya maziwa ya mataifa,Utanyonya matiti ya wafalme;Nawe utajua ya kuwa mimi, BWANA, ni mwokozi wako,Na mkombozi wako, Mwenye enzi wa Yakobo.

17. Badala ya shaba nitaleta dhahabu,Na badala; ya chuma nitaleta fedha,Na badala ya mti, shaba,Na badala ya mawe, chuma;Tena nitawafanya wasimamizi wako wawe amani,Na hao wakutozao fedha kuwa haki.

Isa. 60