17. Nao wakamtwaa Absalomu wakamtupa katika shimo kubwa mle msituni, wakaweka juu yake chungu kubwa sana la mawe; kisha Israeli wote wakakimbia kila mtu hemani mwake.
18. Huyo Absalomu alipokuwa yu hai alikuwa ameitwaa na kujiinulia ile nguzo iliyoko bondeni mwa mfalme; kwa maana alisema, Mimi sina mtoto wa kulikumbusha jina langu; akaiita hiyo nguzo kwa jina lake mwenyewe nayo inaitwa ziara la Absalomu hata hivi leo.
19. Basi Ahimaasi, mwana wa Sadoki, akasema, Niende mbio sasa, nikampelekee mfalme habari, jinsi BWANA alivyomlipiza kisasi juu ya adui zake.
20. Yoabu akamwambia, Wewe hutakuwa mchukua habari leo, siku nyingine utachukua habari; lakini leo hutachukua habari, kwa sababu mwana wa mfalme amekufa.
21. Ndipo Yoabu akamwambia Mkushi mmoja, Nenda ukamwambie mfalme hayo uliyoyaona. Na huyo Mkushi akajiinamisha mbele ya Yoabu, akaenda zake mbio.
22. Ndipo Ahimaasi, mwana wa Sadoki, akamwambia Yoabu mara ya pili, Haidhuru, tafadhali nipe ruhusa, nipige mbio na mimi nyuma ya huyo Mkushi. Naye Yoabu akasema, Mbona wewe unataka kupiga mbio, mwanangu, kwa maana hutapata kitu kwa habari hizo unazopeleka?
23. Akasema, Haidhuru, nitapiga mbio. Akamwambia, Haya, piga mbio. Ndipo Ahimaasi akapiga mbio, akishika njia ya uwandani, akampita yule Mkushi.
24. Basi Daudi alikuwa ameketi kati ya malango mawili; mlinzi akapanda juu hata dari ya lile lango hata ukutani, akainua macho yake, akaangalia, na tazama, mtu anakuja mbio peke yake.
25. Mlinzi akalia, akamwambia mfalme. Naye mfalme akasema, Kama yu peke yake, ana habari kinywani mwake. Akaja mbio, akakaribia.
26. Kisha huyo mlinzi akaona mtu mwingine anapiga mbio; mlinzi akamwita bawabu, akasema, Angalia, mtu mwingine anakuja mbio peke yake. Mfalme akasema, Huyu naye analeta habari.
27. Na huyo mlinzi akasema, Nionavyo mimi, kupiga mbio kwake yule wa kwanza ni kama kupiga mbio kwake Ahimaasi, mwana wa Sadoki. Naye mfalme akasema, Yeye ni mtu mwema, anakuja na habari njema.
28. Ahimaasi akainua sauti yake, akamwambia mfalme, Amani. Akainama mbele ya mfalme kifudifudi, akasema, Ahimidiwe BWANA, Mungu wako, aliyewatoa watu hao walioiinua mikono yao juu ya bwana wangu, mfalme.
29. Mfalme akauliza, Je! Yule kijana, Absalomu, yu salama? Ahimaasi akajibu, Yoabu aliponituma mimi mtumishi wa mfalme, mimi mtumishi wako, naliona kishindo kikubwa, lakini sikujua sababu yake.