4. na wewe, ukienda mbele zangu kama alivyokwenda Daudi, baba yako, kwa ukamilifu wa moyo, na kwa adili, kufanya hayo yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu,
5. ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli.
6. Bali mkighairi, mkaacha kunifuata, ninyi na watoto wenu, msizishike sheria zangu na amri zangu, nilizoziweka mbele yenu, tena mkienda na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu,
7. basi nitawakatilia Israeli mbali na nchi hii niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaitupilia mbali na macho yangu, na Israeli watakuwa mithali na neno la tusi katika mataifa yote.
8. Na ijapokuwa nyumba hii imetukuka namna hii, lakini kila apitaye atasituka na kuizomea; nao watasema, Kwa nini BWANA ameitenda nchi hii na nyumba hii mambo haya?
9. Na watu watajibu, Kwa sababu walimwacha BWANA, Mungu wao, aliyewatoa baba zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine na kuiabudu na kuitumikia, basi ndiyo sababu BWANA ameleta mabaya haya yote juu yao.
10. Ikawa miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani alizijenga zile nyumba mbili, nyumba ya BWANA na nyumba yake mfalme,
11. (basi Hiramu, mfalme wa Tiro, alikuwa amemletea Sulemani mierezi na miberoshi, na dhahabu, sawasawa na haja zake zote), ndipo mfalme Sulemani akampa Hiramu miji ishirini ya nchi ya Galilaya.
12. Naye Hiramu akatoka Tiro kuitazama hiyo miji Sulemani aliyompa; wala haikumpendcza.
13. Akasema, Miji gani hii uliyonipa, ndugu yangu? Akaiita nchi ya Kabuli, hata leo.
14. Hiramu akamletea mfalme talanta sitini za dhahabu.
15. Na hii ndiyo sababu ya shokoa aliyoitoza mfalme Sulemani; ili kuijenga nyumba ya BWANA, na nyumba yake mwenyewe, na Milo, na ukuta wa Yerusalemu, na Hazori, na Megido, na Gezeri.
16. Farao, mfalme wa Misri, alikuwa amepanda akautwaa Gezeri, na kuuteketeza kwa moto, akawaua Wakanaani waliokaa mjini, akampa zawadi binti yake, mkewe Sulemani.
17. Naye Sulemani akaujenga Gezeri, na Beth-horoni wa chini,
18. na Baalathi, na Tamari ulio nyikani, katika nchi;
19. na miji yote ya hazina iliyokuwa yake Sulemani; na miji ya magari yake, na miji ya watu wake wapandao farasi, na kila alichopenda kujenga Sulemani huko Yerusalemu, na katika Lebanoni, na katika nchi yote ya mamlaka yake.