1. Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu katika habari za shamba lake la mizabibu.Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu,Kilimani penye kuzaa sana;
2. Akafanya handaki kulizunguka pande zote,Akatoa mawe yake,Akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri,Akajenga mnara katikati yake,Akachimba shinikizo ndani yake;Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu,Nao ukazaa zabibu-mwitu.
3. Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu.
4. Je! Ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibu-mwitu?
5. Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa kitalu chake, nalo litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa;
6. nami nitaliharibu; wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.
7. Kwa maana shamba la mizabibu la BWANA wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza; akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! Aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe! Alisikia kilio.
8. Ole wao waongezao nyumba baada ya nyumba, na kuweka shamba karibu na shamba, hata hapana nafasi tena, nanyi hamna budi kukaa peke yenu kati ya nchi!
9. BWANA wa majeshi asema katika masikio yangu, Hakika majumba mengi yatakuwa ukiwa, naam, majumba makubwa, mazuri, yatakuwa hayana watu.
10. Kwa maana shamba la mizabibu la eka kumi litatoa bathi moja tu, na homeri ya mbegu itatoa efa tu.
11. Ole wao waamkao asubuhi na mapema, wapate kufuata kileo; wakishinda sana hata usiku wa manane mpaka mvinyo imewaka kama moto ndani yao!
12. Na kinubi, na zeze, na matari, na filimbi, na mvinyo, zote ziko katika karamu zao; lakini hawaiangalii kazi ya BWANA wala kuyafikiri matendo ya mikono yake.