Isa. 38:10-19 Swahili Union Version (SUV)

10. Nalisema, Katika usitawi wa siku zangu nitakwenda kuingia malango ya kuzimu;Nimenyimwa mabaki ya miaka yangu.

11. Nalisema, Sitamwona BWANA, yeye BWANA, katika nchi ya walio hai;Sitamwona mwanadamu tena pamoja na hao wakaao duniani.

12. Kao langu limeondolewa kabisa,limechukuliwa kama hema ya mchungaji;Nimekunja maisha yangu kama mfumaji;atanikatilia mbali na kitanda cha mfumi;Tangu mchana hata usiku wanimaliza.

13. Nalijituliza hata asubuhi;kama simba, aivunja mifupa yangu yote;Tangu mchana hata usiku wanimaliza.

14. Kama mbayuwayu au korongo ndivyo nilivyolia;Naliomboleza kama hua;macho yangu yamedhoofu kwa kutazama juu;Ee BWANA, nimeonewa, na uwe mdhamini wangu.

15. Niseme nini? Yeye amenena nami,na yeye mwenyewe ametenda hayo;Nitakwenda polepole miaka yangu yote,kwa sababu ya uchungu wa nafsi yangu.

16. Ee Bwana, kwa mambo hayo watu huishi;Na uhai wa roho yangu u katika hayo yote;Kwa hiyo uniponye na kunihuisha.

17. Tazama; nalikuwa na uchungu mwingi kwa ajili ya amani yangu;Lakini kwa kunipenda umeniokoa na shimo la uharibifu;Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako.

18. Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu;mauti haiwezi kukuadhimisha;Wale washukao shimoni hawawezi kuitarajia kweli yako.

19. Aliye hai, naam, aliye hai, ndiye atakayekusifu, kama mimi leo;Baba atawajulisha watoto kweli yako.

Isa. 38