2 Sam. 3:21-30 Swahili Union Version (SUV)

21. Kisha Abneri akamwambia Daudi, Nitaondoka, niende zangu; nami nitamkusanyia bwana wangu mfalme Israeli wote, ili wafanye agano nawe, ukamiliki juu ya wote inaowatamani roho yako. Basi Daudi akamruhusu Abneri; naye akaenda zake kwa amani.

22. Na tazama, watumishi wa Daudi pamoja na Yoabu walitoka jeshini, wakaleta mateka mengi pamoja nao; lakini Abneri hakuwako Hebroni kwa Daudi; maana alikuwa amemruhusu, naye amekwisha kwenda zake kwa amani.

23. Hata Yoabu, na jeshi lote waliokuwa pamoja naye, walipofika, watu wakamwambia Yoabu, wakisema, Abneri, mwana wa Neri, alikuja kwa mfalme, naye amemruhusu, naye amekwenda zake kwa amani.

24. Basi Yoabu akamwendea mfalme, akasema, Umefanyaje? Tazama, Abneri amekuja kwako; mbona umemruhusu, naye amekwisha kwenda zake?

25. Wewe wamjua Abneri, mwana wa Neri, ya kuwa alikuja ili kukudanganya, apate kujua kutoka kwako, na kuingia kwako, akajue yote uyatendayo.

26. Naye Yoabu alipotoka kwa Daudi, akapeleka wajumbe kumfuata Abneri, wakamrudisha kutoka kisima cha Sira; lakini Daudi alikuwa hana habari.

27. Basi Abneri alipokuwa amerudi Hebroni, Yoabu akamchukua kando hata katikati ya lango, ili aseme naye kwa faragha; akampiga mkuki wa tumbo huko, hata akafa; kwa ajili ya damu ya Asaheli, ndugu yake.

28. Hata baadaye Daudi aliposikia, akasema, Mimi na ufalme wangu hatuna hatia milele mbele za BWANA, kwa sababu ya damu ya Abneri, mwana wa Neri;

29. na imwangukie Yoabu kichwani pake, na nyumba yote ya babaye, tena hiyo nyumba ya Yoabu isikose kuwa na mtu mwenye kutoka damu, au aliye na ukoma, au mwenye kutegemea fimbo, au mwenye kuanguka kwa upanga au mwenye kuhitaji chakula.

30. Basi Yoabu, na Abishai nduguye, walimwua Abneri, kwa sababu yeye alimwua ndugu yao Asaheli katika vita huko Gibeoni.

2 Sam. 3