3. Daudi naye akawapandisha watu wake waliokuwa pamoja naye, kila mtu na watu wa nyumbani mwake; wakakaa katika miji ya Hebroni.
4. Basi watu wa Yuda wakaenda, wakamtia Daudi mafuta huko, awe mfalme juu ya nyumba ya Yuda.Wakamwambia Daudi wakasema, Watu wa Yabesh-gileadi ndio waliomzika Sauli.
5. Basi Daudi akatuma wajumbe kwa watu wa Yabesh-gileadi, na kuwaambia, Na mbarikiwe ninyi na BWANA, kwa kuwa mmemtendea bwana wenu fadhili hii, yaani Sauli, mkamzika.
6. BWANA naye sasa awatendee ninyi fadhili na kweli; mimi nami nitawalipeni fadhili hiyo, kwa sababu mmetenda jambo hilo.
7. Basi sasa, mikono yenu na itiwe nguvu, nanyi iweni mashujaa; maana Sauli, bwana wenu, amekufa, tena nyumba ya Yuda wamenitia mimi mafuta niwe mfalme juu yao.
8. Basi Abneri, mwana wa Neri, amiri wa jeshi la Sauli, alikuwa amemtwaa Ishboshethi, mwana wa Sauli, na kumvusha na kumpeleka Mahanaimu;
9. akamweka awe mfalme juu ya Gileadi, na Waasheri, na Yezreeli, na Efraimu, na Benyamini, na juu ya Israeli wote.
10. (Huyo Ishboshethi, mwana wa Sauli, umri wake alikuwa amepata miaka arobaini alipoanza kutawala juu ya Israeli, akatawala miaka miwili.) Lakini nyumba ya Yuda waliandamana na Daudi.
11. Na wakati Daudi alipotawala Hebroni juu ya nyumba ya Yuda ulikuwa miaka saba na miezi sita.
12. Basi Abneri, mwana wa Neri, na watumishi wa Ishboshethi, mwana wa Sauli, wakatoka Mahanaimu kwenda Gibeoni.
13. Huyo Yoabu naye, mwana wa Seruya, na watumishi wa Daudi, wakatoka, wakakutana nao karibu na ziwa la Gibeoni; wakaketi, hawa upande huu wa ziwa, na hawa upande huu wa ziwa.
14. Abneri akamwambia Yoabu, Tafadhali vijana hawa na waondoke na kucheza mbele yetu. Yoabu akasema, Haya! Na waondoke.
15. Basi wakaondoka, wakaenda upande wa pili kwa hesabu yao watu kumi na wawili wa Benyamini, na wa Ishboshethi, mwana wa Sauli na watu kumi na wawili wa watumishi wa Daudi.
16. Wakakamatana, kila mtu akimshika mwenziwe kichwa chake, na kutia upanga wake katika ubavu wa mwenzake; wakaanguka pamoja; hata mahali pale pakaitwa Helkath-hasurimu, napo ni katika Gibeoni.
17. Vita vile vilikuwa vikali sana siku ile; naye Abneri akashindwa, na watu wa Israeli, mbele ya watumishi wa Daudi.
18. Na wana watatu wa Seruya walikuwako huko, Yoabu, na Abishai, na Asaheli; na Asaheli alikuwa mwepesi wa miguu kama kulungu.