2 Sam. 2:20-32 Swahili Union Version (SUV)

20. Basi Abneri akatazama nyuma yake, akasema, Ni wewe, Asaheli? Akajibu, Ni mimi.

21. Basi Abneri akamwambia, Geuka mkono wa kuume au mkono wa kushoto, ukamshike mmoja wa vijana, ukazitwae silaha zake. Lakini Asaheli hakukubali kugeuka na kuacha kumfuata.

22. Abneri akamwambia Asaheli mara ya pili, Geuka, acha kunifuatia mimi; kwa nini nikupige hata chini? Hapo ningewezaje kuinua uso wangu mbele ya Yoabu, ndugu yako?

23. Lakini akakataa kugeuka; kwa hiyo Abneri akampiga tumboni kwa ncha ya nyuma ya mkuki wake, ule mkuki ukamtoka kwa nyuma; naye akaanguka hapo, akafa papo hapo; ikawa, watu wote waliofika hapo, alipoanguka Asaheli na kufa, wakasimama.

24. Ila Yoabu na Abishai wakamfuatia Abneri; na jua likachwa hapo walipoufikilia mlima wa Ama, uelekeao Gia, katika njia ya nyika ya Gibeoni.

25. Nao wana wa Benyamini wakakusanyika pamoja nyuma ya Abneri, wakawa kikosi kimoja, wakasimama juu ya mlima.

26. Ndipo huyo Abneri akamwita Yoabu, akasema, Je! Upanga uwale watu sikuzote? Je! Hujui ya kwamba utakuwa uchungu mwisho wake? Basi itakuwa hata lini usijewaamuru watu warudi na kuacha kuwafuatia ndugu zao?

27. Naye Yoabu akasema, Aishivyo Mungu, usingalinena, basi asubuhi wangalikwenda zao, wasiwafuatie kila mtu ndugu yake.

28. Basi Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wote wakasimama, wasiwafuatie Israeli tena, wala hawakupigana tena.

29. Wakaenda Abneri na watu wake usiku ule wote kati ya ile Araba; wakavuka Yordani, wakapita kati ya Bithroni yote, wakaja Mahanaimu.

30. Akarudi Yoabu naye kutoka kumfuatia Abneri; na alipokwisha kuwakusanya watu wote pamoja, wa hao watumishi wa Daudi walipungukiwa na watu kumi na kenda pamoja na Asaheli.

31. Ila watumishi wa Daudi walikuwa wamewapiga watu wa Benyamini, na watu wa Abneri, hata wakafa watu mia tatu na sitini.

32. Nao wakamwinua Asaheli, wakamzika katika kaburi la baba yake, lililokuwako Bethlehemu. Yoabu na watu wake wakaenda usiku kucha, wakapambazukiwa huko Hebroni.

2 Sam. 2