9. Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu.
10. Akasema, Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata; la hukuniona, hulipati.
11. Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli.
12. Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili.
13. Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani.
14. Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi BWANA, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka.
15. Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake.
16. Wakamwambia, Angalia, wako hapa pamoja nasi watumishi wako watu hamsini walio hodari; waende, twakuomba, wamtafute bwana wako; isiwe labda roho ya BWANA imemtwaa na kumtupa juu ya mlima mmoja, au katika bonde moja. Akasema, Msiwatume.
17. Wakamsisitiza hata akaona haya, akasema, Haya! Watumeni. Basi wakatuma watu hamsini; nao wakatafuta siku tatu, wasimwone.
18. Wakamrudia, alipokuwa anakawia Yeriko; akawaambia, Je! Mimi sikuwaambia, Msiende?
19. Watu wa mjini wakamwambia Elisha, Angalia, twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo; lakini maji yake hayafai, na nchi huzaa mapooza.
20. Akasema, Nileteeni chombo kipya, mtie chumvi ndani yake. Wakamletea.
21. Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, BWANA asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza.
22. Hivyo yale maji yakapona hata leo, sawasawa na neno la Elisha alilolinena.
23. Akakwea kutoka huko mpaka Betheli; naye alipokuwa akienda njiani, wakatoka vijana katika mji, wakamfanyizia mzaha, wakamwambia, Paa wewe mwenye upaa! Paa wewe mwenye upaa!
24. Akatazama nyuma akawaona, akawalaani kwa jina la BWANA. Wakatoka dubu wawili wa kike mwituni, wakawararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao.