10. Daudi akasema, Aishivyo BWANA, BWANA atampiga; au siku yake ya kufa itampata; atashuka kwenda vitani na kupotea.
11. Hasha! Nisiunyoshe mkono wangu juu ya masihi wa BWANA; lakini sasa tafadhali twaa hili fumo lililo kichwani pake, na hili gudulia la maji, nasi twende zetu.
12. Basi Daudi akalitwaa lile fumo, na lile gudulia la maji, kichwani pa Sauli; nao wakaenda zao, wala hapana mtu aliyeliona jambo hili wala kulijua, wala kuamka; maana wote walikuwa wamelala; kwa kuwa usingizi mzito kutoka kwa BWANA umewaangukia.
13. Kisha Daudi akaenda ng’ambo ya pili, akasimama juu ya kilima, mbali sana; palipokuwapo nafasi tele katikati yao;
14. naye Daudi akawapigia kelele watu wale, na Abneri, mwana wa Neri, akasema, Abneri, hujibu? Ndipo Abneri akajibu, akasema, U nani wewe unayemlilia mfalme?
15. Naye Daudi akamwambia Abneri, Wewe si mtu shujaa? Tena ni nani aliye sawa na wewe katika Israeli? Mbona, basi, hukumlinda bwana wako, huyo mfalme? Kwa maana mtu mmoja aliingia ili amwangamize mfalme, bwana wako?
16. Jambo hili ulilolitenda si jema. Aishivyo BWANA, mmestahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, masihi wa BWANA. Haya basi! Tazameni, liko wapi fumo la mfalme, na gudulia la maji lililokuwa kichwani pake?
17. Naye Sauli akaitambua sauti ya Daudi, akasema, Hii ndiyo sauti yako, Daudi, mwanangu? Daudi akasema, Ndiyo, ni sauti yangu, bwana wangu, mfalme.
18. Akasema, Bwana wangu ananiwinda mimi mtumishi wake kwa sababu gani? Nimefanya nini mimi? Ni uovu gani nilio nao mkononi mwangu?
19. Basi sasa, nakusihi, bwana wangu, mfalme, na asikie maneno ya mtumishi wake. Ikiwa ni BWANA aliyekuondokesha juu yangu, na akubali sadaka; bali ikiwa ni wanadamu, na walaaniwe mbele za BWANA; kwa sababu wamenifukuza leo, nisishikamane na urithi wa BWANA, wakisema, Enenda, katumikie miungu mingine.
20. Basi sasa, isianguke damu yangu chini mbali na uso wa BWANA; maana mfalme wa Israeli ametoka ili kutafuta uhai wangu, kama vile mtu awindavyo kware mlimani.
21. Ndipo Sauli akasema, Nimekosa; rudi, Daudi, mwanangu; maana sitakudhuru tena, kwa kuwa maisha yangu yalikuwa na thamani machoni pako leo; angalia, nimetenda upumbavu, nimekosa sana.
22. Daudi akajibu, akasema, Litazame fumo hili, Ee mfalme! Kijana mmoja na avukie huku, alitwae.
23. Naye BWANA atamlipa kila mtu haki yake, na uaminifu wake; maana BWANA amekutia mikononi mwangu leo, nami nalikataa kuunyosha mkono wangu juu ya masihi wa BWANA.
24. Tena, angalia, kama vile maisha yako yalivyokuwa na thamani machoni pangu, kadhalika na maisha yangu na yawe na thamani machoni pa BWANA, akaniokoe katika shida zote.
25. Ndipo Sauli akamwambia Daudi, Ubarikiwe, Daudi, mwanangu; utatenda mambo makuu, tena hakika yako utashinda. Basi, Daudi akaenda zake; Sauli naye akarudi kwao.