1 Sam. 14:13-27 Swahili Union Version (SUV)

13. Basi Yonathani akapanda kwa mikono na miguu yake, na mchukua silaha nyuma yake; na hao watu wakaanguka mbele ya Yonathani; na huyo mchukua silaha zake akawaua nyuma yake.

14. Na uuaji huo wa kwanza walioufanya Yonathani na mchukua silaha zake, ulipata kama watu ishirini, katika nafasi kama nusu ya kiwanja kiwezacho kulimwa katika siku nzima.

15. Kukawa na tetemeko katika marago, na katika mashamba, na katikati ya watu wote; watu wa ngomeni, na watekaji wa nyara, wakatetemeka nao; hata na nchi ikatetemeka pia; basi kulikuwa na tetemeko kubwa mno.

16. Nao wale walinzi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaangalia, na tazama, mkutano ule ulikuwa ukitoweka, na watu walikuwa wakienda huko na huko.

17. Ndipo Sauli akawaambia watu waliokuwa pamoja naye, Haya! Hesabuni sasa, mkaone ni nani aliyeondoka kwetu. Nao walipokwisha hesabu, tazama Yonathani na yeye aliyechukua silaha zake hawapo.

18. Basi Sauli akamwambia Ahiya, Lilete hapa sanduku la Mungu. Kwa kuwa hilo sanduku la Mungu wakati huo lilikuwapo pamoja na wana wa Israeli.

19. Ikawa Sauli alipokuwa katika kusema na kuhani, hayo makelele katika marago ya Wafilisti yakaendelea na kuzidi; basi Sauli akamwambia kuhani, Rudisha mkono wako.

20. Naye Sauli na watu wote waliokuwapo pamoja naye wakakusanyika, wakaenda vitani; na tazama, huko upanga wa kila mtu ulikuwa juu ya mwenziwe, kukawa fujo tele kabisa.

21. Basi na wale Waebrania waliokuwa pamoja na Wafilisti tangu zamani, wale waliopanda pamoja nao mpaka maragoni toka nchi iliyozunguka; watu hao nao wakageuka kuwa upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani.

22. Na vile vile watu wote wa Israeli waliokuwa wamejificha katika nchi ya milima milima ya Efraimu, waliposikia ya kwamba Wafilisti wamekimbia, hata hao nao wakawafuatia mbio vitani.

23. Hivyo BWANA akawaokoa Israeli siku ile; na vita vikapita mbele karibu na Beth-aveni. Wakati huo mbele ya wana wa Israeli.

24. Nao watu wa Israeli walisumbuka sana siku ile; lakini Sauli alikuwa amewaapisha watu, akisema, Na alaaniwe mtu awaye yote alaye chakula cho chote hata jioni, nipate kujilipiza kisasi juu ya adui zangu. Basi hakuna mtu miongoni mwa watu aliyeonja chakula.

25. Nao watu wote wakaingia mwituni; na humo mlikuwa na asali juu ya nchi.

26. Na hapo watu walipokwisha kuingia mwituni, tazama, hiyo asali ilikuwa ikidondoka; walakini hakuna mtu hata mmoja aliyetia mkono wake kinywani; kwa sababu hao watu walikuwa wakikiogopa kile kiapo.

27. Ila Yonathani hakusikia, hapo babaye alipowaagiza watu kwa kiapo; basi yeye akainyosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake, na kuichovya katika sega la asali, kisha akatia mkono wake kinywani; na macho yake yakatiwa nuru.

1 Sam. 14