1 Fal. 11:10-26 Swahili Union Version (SUV)

10. akamwamuru katika habari ya jambo lilo hilo asifuate miungu mingine; lakini yeye hakuyashika aliyoyaamuru BWANA.

11. Kwa hiyo BWANA akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako.

12. Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako.

13. Lakini sitauondoa ufalme wote pia; nitampa mwana wako kabila moja, kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu niliouchagua.

14. Ndipo BWANA akamwondokeshea Sulemani adui, Hadadi Mwedomi; yeye alikuwa wa wazao wake mfalme wa Edomu.

15. Kwa maana ikawa, Daudi alipokuwako Edomu, naye Yoabu, mkuu wa jeshi, amepanda awazike waliouawa, akiisha kumpiga kila mwanamume wa Edomu,

16. (kwa kuwa Yoabu alikaa huko miezi sita pamoja na Israeli wote, hata alipompoteza kila mwanamume wa Edomu);

17. yule Hadadi alikimbia, yeye na Waedomi wengine, watumishi wa baba yake, pamoja naye, waende Misri; yule Hadadi akali ni mtoto mdogo.

18. Wakaondoka katika Midiani, wakafika Parani; wakachukua pamoja nao watu toka Parani, wakafika Misri, kwa Farao mfalme wa Misri; aliyempa nyumba, akamwamria vyakula, akampa mashamba.

19. Hadadi akapendeza sana machoni pa Farao, hata akamwoza umbu la mkewe, umbu la Tapenesi aliyekuwa malkia.

20. Naye huyo umbu la Tapenesi akamzalia Genubathi mwanawe, ambaye Tapenesi alimlea nyumbani mwa Farao; naye Genubathi akawako nyumbani mwa Farao pamoja na wana wa Farao.

21. Naye Hadadi aliposikia huko Misri ya kuwa Daudi amelala na babaze, na Yoabu, jemadari wa jeshi, amekufa, Hadadi akamwambia Farao, Unipe ruhusa, niende mpaka nchi yangu.

22. Farao akamwambia, Umekosa nini kwangu, hata, tazama, unatafuta kuirudia nchi yako? Akajibu, Hakuna, lakini unipe ruhusa tu.

23. Tena, Mungu akamwondokeshea adui mwingine, Rezoni mwana wa Eliada, aliyemkimbia bwana wake Hadadezeri mfalme wa Soba,

24. naye akakusanya watu, akawa mkuu wa jeshi, hapo Daudi alipowaua hao watu wa Soba; wakaenda Dameski, wakakaa humo, na kumiliki huko Dameski.

25. Naye akawa adui wa Israeli siku zote za Sulemani, zaidi ya madhara yake Hadadi; naye akawachukia Israeli, akamiliki juu ya Shamu.

26. Na Yeroboamu wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumwa wake Sulemani; ambaye jina lake mamaye aliitwa Serua, mwanamke aliyefiwa na mumewe; yeye naye akainua mkono wake juu ya mfalme.

1 Fal. 11