Yer. 22:5-23 Swahili Union Version (SUV)

5. Lakini kama hamtaki kusikia maneno haya, mimi naapa kwa nafsi yangu, asema BWANA, ya kuwa nyumba hii itakuwa ukiwa.

6. Kwa maana BWANA asema hivi, katika habari ya nyumba ya mfalme wa Yuda;Wewe u Gileadi kwangu,na kichwa cha Lebanoni;Ila hakika nitakufanya kuwa jangwa,na miji isiyokaliwa na watu.

7. Nami nitakufanyia tayari watu wenye kuharibu,kila mtu na silaha zake;Nao watakata mierezi miteule yako,na kuitupa motoni.

8. Na mataifa mengi watapita karibu na mji huu, nao watasema kila mtu na jirani yake, Nini maana yake BWANA kuutenda hivi mji huu mkubwa?

9. Ndipo watakapojibu, Ni kwa sababu waliliacha agano la BWANA, Mungu wao, wakaabudu miungu mingine, na kuitumikia.

10. Msimlilie aliyekufa, wala msimwombolezee,Bali mlilieni huyo aendaye zake mbali;Kwa maana yeye hatarudi tena,Wala hataiona nchi aliyozaliwa.

11. Maana BWANA asema hivi, katika habari za Shalumu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; aliyemiliki badala ya Yosia, baba yake, yeye aliyetoka mahali hapa; Hatarudi huku tena;

12. bali katika mahali pale walipomchukua mateka ndipo atakapokufa, wala hataiona nchi hii tena kamwe.

13. Ole wake aijengaye nyumba yake kwa uovu!Na vyumba vyake kwa udhalimu!Atumiaye utumishi wa mwenzake bila ujira,Wala hampi mshahara wake;

14. Asemaye, Nitajijengea nyumba pana na vyumba vipana;Naye hujikatia madirisha;Na kuta zake zimefunikwa kwa mierezi,Na kupakwa rangi nyekundu.

15. Je! Utatawala kwa sababu unashindana na watu kwa mierezi? Baba yako, je! Hakula na kunywa, na kufanya hukumu na haki? Hapo ndipo alipofanikiwa.

16. Alihukumu maneno ya maskini na mhitaji; hapo ndipo alipofanikiwa. Je! Huku siko kunijua, asema BWANA?

17. Bali macho yako na moyo wako hauna utakalo ila kutamani, na kumwaga damu isiyo na hatia, na kudhulumu, na kutenda jeuri.

18. Basi, BWANA asema hivi, katika habari ya Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; Hawatamwombolezea, wakisema, Aa! Ndugu yangu; au, Aa! Dada yangu; wala hawatamlilia, wakisema, Aa! Bwana wangu; au, Aa! Utukufu wake.

19. Atazikwa maziko ya punda, akibururwa, na kutupwa nje ya malango ya Yerusalemu.

20. Haya panda Lebanoni, ukalieUpalize sauti yako katika Bashani;Ukalie kutoka Abarimu;Maana wapenzi wako wote wameangamia.

21. Mimi nalisema nawe wakati wa kufanikiwa kwako; lakini ulisema, Sitaki kusikia. Hii ndiyo iliyokuwa desturi yako tangu ujana wako, kutokuitii sauti yangu.

22. Upepo utawalisha wachungaji wako wote, na wapenzi wako watakwenda kufungwa; hakika wakati huo utatahayarika, na kufadhaika kwa sababu ya uovu wako wote.

23. Wewe ukaaye Lebanoni,Ufanyaye kioto chako katika mierezi,Utakuwa na hali ya kuhurumiwa sana,Upatapo utungu kama wa mwanamke azaaye.

Yer. 22