6. Nimekatilia mbali mataifa, buruji zao zina ukiwa; nimeziharibu njia kuu zao, hata hapana mmoja apitaye; miji yao imeangamizwa; hamna mtu hata mmoja, wala hapana akaaye huko.
7. Nalisema, Hakika utaniogopa, utakubali kurudiwa; ili yasikatiliwe mbali makao yake, sawasawa ya yote niliyoagiza katika habari zake; lakini waliondoka mapema na kuyaharibu matendo yao yote.
8. Basi ningojeni, asema BWANA, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu; kwa maana dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wangu.
9. Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la BWANA, wamtumikie kwa nia moja.
10. Maana toka nchi iliyo mbali na mito ya Kushi, waniombao dua, yaani, binti za watu wangu waliotawanyika, wataleta matoleo yangu.
11. Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu.
12. Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la BWANA.
13. Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya.
14. Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli;Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu.
15. BWANA ameziondoa hukumu zako,Amemtupa nje adui yako;Mfalme wa Israeli, naam, yeye BWANA, yu katikati yako;Hutaogopa uovu tena.
16. Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa,Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee.
17. BWANA, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa;Atakushangilia kwa furaha kuu,Atakutuliza katika upendo wake,Atakufurahia kwa kuimba.
18. Nitawakusanya wanaousikitikia mkutano wa ibada, hao waliokuwa wa kwako; ambao mzigo uliokuwa juu yake ulikuwa fedheha kwao.