34. Basi Raheli alikuwa amevitwaa vile vinyago ameviweka katika matandiko ya ngamia, na kuvikalia. Labani akapapasa hema yote wala hakuviona.
35. Naye Raheli akamwambia babaye, Bwana wangu asikasirike kwa sababu siwezi kuinuka mbele yako, maana nimeshikwa na mambo ya kike. Akatafuta, wala hakuviona vile vinyago.
36. Yakobo akakasirika, akagombana na Labani. Yakobo akajibu, akamwambia Labani, N’nini hatia yangu? Nayo ni nini dhambi yangu, hata ukanifuatia namna hii?
37. Umepapasa-papasa vyombo vyangu vyote; ni kitu gani ulichokiona cha nyumbani mwako? Kiweke hapa mbele ya ndugu zangu, na ndugu zako, wakaamue kati yetu.
38. Miaka hii ishirini nimekaa kwako; kondoo zako wala mbuzi zako wake hawakuharibu mimba wala waume katika wanyama wako sikuwala.
39. Kilichoraruliwa na hayawani sikukuletea, mimi mwenyewe nimetwaa hasara yake, wewe umekidai katika mkono wangu, ikiwa kilichukuliwa mchana, au ikiwa kilichukuliwa usiku.
40. Hii ilikuwa hali yangu; mchana jua likanipata, na baridi usiku, usingizi ukanitoka machoni mwangu.
41. Miaka hii ishirini nimekaa nyumbani mwako; nilikutumikia miaka kumi na minne kwa binti zako wawili, na miaka sita kwa wanyama wako, nawe umebadili mshahara wangu mara kumi.