Mit. 14 Swahili Union Version (SUV)

1. Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake;Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.

2. Yeye aendaye kwa unyofu wake humcha BWANA;Bali aliye mkaidi katika njia zake humdharau.

3. Katika kinywa cha mpumbavu mna fimbo ya kiburi,Bali midomo ya wenye hekima huwahifadhi.

4. Zizi ni safi ambapo hapana ng’ombe;Bali nguvu za ng’ombe zaleta faida nyingi.

5. Shahidi mwaminifu hatasema uongo;Bali shahidi wa uongo, pumzi zake ni uongo.

6. Mwenye dharau hutafuta hekima, asiipate;Bali maarifa huwa mepesi kwa mwenye ufahamu.

7. Toka mbele ya uso wa mpumbavu,Maana hutaona kwake midomo ya maarifa.

8. Akili za mwenye busara ni kujua njia yake;Lakini upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu.

9. Wapumbavu huidharau hatia;Bali upo upendeleo kwa wenye haki.

10. Moyo huujua uchungu wa nafsi yake,Wala mgeni haishiriki furaha yake.

11. Nyumba ya mtu mbaya itabomolewa;Bali hema ya mwenye haki itafanikiwa.

12. Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu,Lakini mwisho wake ni njia za mauti.

13. Hata wakati wa kucheka moyo huwa na huzuni;Na mwisho wa furaha ni uzito wa moyo.

14. Ageukaye moyoni hushiba njia zake mwenyewe;Na mtu mwema ataridhika nafsini mwake.

15. Mjinga huamini kila neno;Bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.

16. Mwenye hekima huogopa, akajitenga na uovu;Bali mpumbavu ana ufidhuli, na kujitumai.

17. Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga;Na mtu mwenye hila mbaya huzirwa.

18. Wajinga hurithi upumbavu;Bali wenye busara huvikwa taji ya maarifa.

19. Wabaya huinama mbele ya wema,Na wasio haki malangoni mwao wenye haki.

20. Maskini huchukiwa hata na jirani yake;Bali tajiri ana rafiki wengi.

21. Amdharauye mwenzake afanya dhambi;Bali amhurumiaye maskini ana heri.

22. Je! Hawakosi wawazao mabaya?Bali fadhili na kweli zina wao wawazao mema.

23. Katika kila kazi mna faida;Bali maneno ya midomo huleta hasara tu.

24. Taji ya wenye hekima ni mali zao;Bali upumbavu wa wajinga ni upumbavu tu.

25. Shahidi wa kweli huponya nafsi za watu;Bali atoaye uongo hudanganya.

26. Kumcha BWANA ni tumaini imara;Watoto wake watakuwa na kimbilio.

27. Kumcha BWANA ni chemchemi ya uzima,Ili kuepukana na tanzi za mauti.

28. Utukufu wa mfalme ni wingi wa watu wake;Bali uchache wa watu ni uharibifu wa mkuu wao.

29. Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi;Bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu.

30. Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili;Bali husuda ni ubovu wa mifupa.

31. Amwoneaye maskini humsuta Muumba wake;Bali yeye awahurumiaye wahitaji humheshimu.

32. Mtu mbaya husukumwa chini katika kutenda mabaya kwake;Bali mwenye haki ana matumaini katika kufa kwake.

33. Hekima hukaa katika moyo wake mwenye ufahamu;Bali yaliyo ndani ya wapumbavu hudhihirika.

34. Haki huinua taifa;Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.