Mit. 13 Swahili Union Version (SUV)

1. Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye;Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo.

2. Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake;Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri.

3. Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake;Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu.

4. Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu;Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa.

5. Mwenye haki huchukia kusema uongo;Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu.

6. Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake;Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi.

7. Kuna mtu mwenye kujitajirisha, lakini hana kitu;Kuna ajifanyaye kuwa maskini, lakini ana mali nyingi.

8. Dia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake;Bali mtu maskini hasikii ogofyo lo lote.

9. Nuru ya mwenye haki yang’aa sana;Bali taa ya mtu mbaya itazimika.

10. Kiburi huleta mashindano tu;Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.

11. Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka;Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa.

12. Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua.Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.

13. Kila alidharauye neno hujiletea uharibifu;Bali yeye aiogopaye amri atapewa thawabu.

14. Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima,Ili kuepukana na tanzi za mauti.

15. Ufahamu mwema huleta upendeleo;Bali njia ya haini huparuza.

16. Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa;Bali mpumbavu hueneza upumbavu.

17. Mjumbe mbaya huanguka maovuni;Bali mjumbe mwaminifu ni afya.

18. Umaskini na fedheha zitampata yeye akataaye kurudiwa;Bali yeye aangaliaye maonyo ataheshimiwa.

19. Haja iliyopatikana ni tamu nafsini mwa mtu;Bali kujitenga na maovu ni chukizo kwa wapumbavu.

20. Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima;Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.

21. Uovu huwaandamia wenye dhambi;Bali mwenye haki atalipwa mema.

22. Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi;Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki.

23. Chakula kingi chapatikana kwa ukulima wa maskini;Bali viko viharibiwavyo kwa sababu ya dhuluma.

24. Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe;Bali yeye ampendaye humrudi mapema.