Mit. 10 Swahili Union Version (SUV)

Mithali za Sulemani.

KITABU CHA PILI

1. Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye;Bali mwana mpumbavu ni mzigo wa mamaye.

2. Hazina za uovu hazifaidii kitu;Bali haki huokoa na mauti.

3. BWANA hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa;Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali.

4. Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini;Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.

5. Akusanyaye wakati wa hari ni mwana mwenye hekima;Bali asinziaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha.

6. Baraka humkalia mwenye haki kichwani;Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu.

7. Kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka;Bali jina la mtu mwovu litaoza.

8. Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo;Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.

9. Aendaye kwa unyofu huenda salama;Bali apotoshaye njia zake atajulikana.

10. Akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko;Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.

11. Kinywa chake mwenye haki ni chemchemi ya uzima;Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu,

12. Kuchukiana huondokesha fitina;Bali kupendana husitiri makosa yote.

13. Hekima hupatikana midomoni mwa mwenye ufahamu;Bali fimbo hufaa kwa mgongo wake asiye na ufahamu.

14. Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa;Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu.

15. Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu;Uangamivu wa maskini ni umaskini wao.

16. Kazi yake mwenye haki huuelekea uzima;Mazao ya wabaya huuelekea dhambi.

17. Akubaliye kurudiwa huwa katika njia ya uzima;Bali yeye aachaye maonyo hukosa.

18. Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo,Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.

19. Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu;Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.

20. Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha teule;Moyo wa mtu mbaya haufai kitu.

21. Midomo ya mwenye haki hulisha watu wengi;Bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu.

22. Baraka ya BWANA hutajirisha,Wala hachanganyi huzuni nayo.

23. Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo;Bali mtu mwenye ufahamu ana hekima.

24. Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia;Na wenye haki watapewa matakwa yao.

25. Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena;Bali mwenye haki ni msingi wa milele.

26. Kama siki menoni, na kama moshi machoni,Ndivyo alivyo mtu mvivu kwao wamtumao.

27. Kumcha BWANA kwaongeza siku za mtu;Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.

28. Matumaini yao wenye haki yatakuwa furaha;Bali kutaraji kwao wasio haki kutapotea.

29. Njia ya BWANA ni kimbilio lake mtu mkamilifu;Bali ni uharibifu kwao watendao maovu.

30. Mwenye haki hataondolewa milele;Bali wasio haki hawatakaa katika nchi.

31. Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima;Bali ulimi wa ukaidi utakatiliwa mbali.