1. Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa;Bali yeye achukiaye kulaumiwa ni kama mnyama.
2. Mtu mwema atapata upendeleo kwa BWANA;Bali mtu wa hila atahukumiwa naye.
3. Mtu hatathibitika kwa njia ya uovu;Shina la mwenye haki halitaondolewa kamwe.
4. Mwanamke mwema ni taji ya mumewe;Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake.
5. Mawazo ya mwenye haki ni adili;Bali mashauri ya mtu mwovu ni hadaa.
6. Maneno ya waovu huotea damu;Bali kinywa cha wanyofu kitawaokoa.
7. Waovu huangamia, hata hawako tena;Bali nyumba ya mwenye haki itasimama.
8. Mtu atasifiwa kwa kadiri ya akili zake;Bali mwenye moyo wa ukaidi atadharauliwa.
9. Afadhali mtu anayedharauliwa, ikiwa ana mtumwa,Kuliko ajisifuye, ikiwa anahitaji chakula.
10. Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake;Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili.
11. Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele;Bali afuataye mambo ya upuzi hana ufahamu.
12. Asiye haki hutamani nyavu za wabaya;Bali shina lao wenye haki huleta matunda.
13. Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya;Bali mwenye haki atatoka katika taabu.
14. Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake;Na atarudishiwa matendo ya mikono yake.
15. Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe;Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.
16. Ghadhabu ya mpumbavu hujulika mara;Bali mtu mwerevu husitiri aibu.
17. Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki;Bali shahidi wa uongo hutamka hila.
18. Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga;Bali ulimi wa mwenye haki ni afya.
19. Mdomo wa kweli utathibitishwa milele;Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.
20. Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu;Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha.
21. Mwenye haki hatapatikana na msiba wo wote;Bali wasio haki watajazwa mabaya.
22. Midomo ya uongo ni chukizo kwa BWANA;Bali watendao uaminifu ndio furaha yake.
23. Mwanadamu mwenye busara husitiri maarifa;Bali moyo wa wapumbavu hutangaza upumbavu.
24. Mkono wa mwenye bidii utatawala;Bali mvivu atalipishwa kodi.
25. Uzito katika moyo wa mtu huuinamisha;Bali neno jema huufurahisha.
26. Mwenye haki ni kiongozi cha mwenzake;Bali njia ya wasio haki huwakosesha.
27. Mtu mvivu hapiki mawindo yake;Bali mwenye bidii anazo mali za thamani.