Mit. 11 Swahili Union Version (SUV)

1. Mizani ya hadaa ni chukizo kwa BWANA;Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza.

2. Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu;Bali hekima hukaa na wanyenyekevu.

3. Ukamilifu wao wenye haki utawaongozaBali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza.

4. Mali hazifaidii kitu siku ya ghadhabu;Bali haki huokoa na mauti.

5. Haki yake mtu mkamilifu itamwongoza njia yake;Bali mtu mwovu ataanguka kwa uovu wake.

6. Haki yao wenye haki itawaokoa;Bali wafanyao fitina watanaswa kwa hila yao wenyewe.

7. Mtu mwovu atakapokufa, taraja lake lapotea;Na matumaini ya uovu huangamia.

8. Mwenye haki huokolewa katika dhiki,Na mtu mwovu ataiingia badala yake.

9. Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake;Bali wenye haki watapona kwa maarifa.

10. Wenye haki wasitawipo, mji hufurahi;Waovu waangamiapo, watu hupiga kelele.

11. Mji hutukuzwa kwa mbaraka wa mwenye haki;Bali mji hupinduliwa kwa kinywa cha mwovu.

12. Asiye na akili humdharau mwenziwe;Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza.

13. Mwenye kitango akisingizia hufunua siri;Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.

14. Pasipo mashauri taifa huanguka;Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.

15. Amdhaminiye mgeni hakosi ataumia;Achukiaye mambo ya dhamana yu salama.

16. Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima;Na watu wakali hushika mali siku zote.

17. Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake;Aliye mkali hujisumbua mwili wake.

18. Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu;Apandaye haki ana thawabu ya hakika.

19. Haki huelekea uzima;Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe.

20. Wenye kuhalifu moyoni ni chukizo kwa BWANA;Walio wakamilifu katika njia zao humpendeza.

21. Hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu;Bali wazao wa wenye haki wataokoka.

22. Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe,Kadhalika mwanamke mzuri asiye na akili.

23. Haja ya mwenye haki ni mema tu;Bali kutaraji kwake mtu mwovu ni ghadhabu.

24. Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi;Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji.

25. Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa;Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe.

26. Awanyimaye watu nafaka, watu watamlaani;Auzaye nafaka, baraka itakuwa kichwani pake.

27. Atafutaye mema kwa bidii hutafuta fadhili;Atafutaye madhara, hayo yatamjia.

28. Azitegemeaye mali zake ataanguka;Mwenye haki atasitawi kama jani.

29. Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo;Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili.

30. Mazao ya mwenye haki ni mti wa uzima;Na mwenye hekima huvuta roho za watu.