2. BWANA, aliyekufanya, na kukuumba toka tumboni, yeye atakayekusaidia, asema hivi; Usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na wewe, Yeshuruni, niliyekuchagua.
3. Kwa maana nitamimina maji juu yake aliye na kiu, na vijito vya maji juu ya mahali pakavu; nitamwaga roho yangu juu ya wazao wako, na baraka yangu juu yao utakaowazaa;
4. nao watatokea katika manyasi, kama mierebi karibu na mifereji ya maji.
5. Mmoja atasema, Mimi ni wa BWANA; na mwingine atajiita kwa jina la Yakobo; na mwingine ataandika juu ya mkono wake, Kwa BWANA, na kujiita kwa jina la Israeli.
6. BWANA, Mfalme wa Israeli, Mkombozi wako, BWANA wa majeshi, asema hivi; Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho; zaidi yangu mimi hapana Mungu.
7. Naye ni nani kama mimi atakayeita, na kuyahubiri haya, na kunitengenezea, tangu nilipowaweka watu wa kale? Na mambo yanayokuja na yatakayotokea, wayatangaze.
8. Msiogope wala msifanye hofu; je! Sikukuhubiri haya zamani na kuyaonyesha? Na ninyi ni mashahidi wangu. Je! Yuko Mungu zaidi yangu mimi? Hakika hapana Mwamba; mimi sijui mwingine.
9. Wachongao sanamu, wote ni ubatili; wala mambo yao yawapendezayo hayatafaa kitu; wala mashahidi wao wenyewe hawaoni, wala hawajui; ili watahayarike.
10. Ni nani aliyejichongea mungu mmoja, au aliyesubu sanamu isiyofaa kitu?
11. Tazama, wenziwe wote watatahayari; na mafundi, hao ni wanadamu; na wakusanyike pamoja, wakasimame; wataogopa na kutahayari pamoja.
12. Mfua chuma hufanza shoka, hufanya kazi kwa makaa, huitengeneza sanamu kwa nyundo, huifanyiza kwa nguvu za mkono wake; naam, huona njaa, nguvu zake zikampungukia; asipokunywa maji huzimia.
13. Seremala hunyosha uzi; huiandika kwa kalamu ya mate; huitengeneza kwa randa, huiandika kwa bikari, huifanza kwa mfano wa mwanadamu, sawasawa na uzuri wa mwanadamu, ili ikae nyumbani.
14. Yeye hujikatia mierezi, hutwaa mtiriza, na mwaloni, hujichagulia mti mmoja katika miti ya msituni; hupanda mvinje, mvua ikausitawisha.
15. Kisha utamfaa mwanadamu kwa kuni; hutwaa kipande, akaota moto; naam, huuwasha moto, akaoka mkate; naam, huufanya mungu, akauabudu; huifanya sanamu ya kuchonga, akaisujudia.