7. Majani yakauka, ua lanyauka;Kwa sababu pumzi ya BWANA yapita juu yake.Yakini watu hawa ni majani.
8. Majani yakauka, ua lanyauka;Bali neno la Mungu wetu litasimama milele.
9. Wewe uuhubiriye Sayuni habari njema,Panda juu ya mlima mrefu;Wewe uuhubiriye Yerusalemu habari njema,Paza sauti kwa nguvu;Paza sauti yako, usiogope;Iambie miji ya Yuda, Tazameni, Mungu wenu.
10. Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa,Na mkono wake ndio utakaomtawalia;Tazameni, thawabu yake i pamoja naye,Na ijara yake i mbele zake.
11. Atalilisha kundi lake kama mchungaji,Atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake;Na kuwachukua kifuani mwake,Nao wanyonyeshao atawaongoza polepole.
12. Ni nani aliyeyapima maji kwa konzi ya mkono wake, na kuzikadiri mbingu kwa shubiri, na kuyashika mavumbi ya dunia katika pishi, na kuipima milima kwa uzani, na vilima kama kwa mizani?
13. Ni nani aliyemwongoza roho ya BWANA, na kumfundisha kwa kuwa mshauri wake?
14. Alifanya shauri na nani, ni nani aliyemwelimisha na kumfunza njia ya hukumu, na kumfunza maarifa, na kumwonyesha njia ya fahamu?
15. Tazama, mataifa ni kama tone la maji katika ndoo, huhesabiwa kuwa kama mavumbi membamba katika mizani; tazama, yeye huvinyanyua visiwa kama ni kitu kidogo sana.
16. Lebanoni nayo hautoshi kwa kuni, wala wanyama wake hawatoshi kwa kafara.
17. Mataifa yote huwa kama si kitu mbele zake; huhesabiwa kwake kuwa duni ya si kitu, na ubatili.
18. Basi, mtamlinganisha Mungu na nani? Au mtamfananisha na mfano wa namna gani?
19. Sanamu fundi mmoja huiyeyusha, na mfua dhahabu huifunika dhahabu, huifulia mikufu ya fedha.
20. Yeye aliye maskini sana hata hawezi kutoa sadaka ya namna hii, huchagua mti usiooza, hujitafutia fundi mstadi wa kusimamisha sanamu ya kuchonga isiyoweza kutikisika.
21. Je! Hamkujua? Hamkusikia? Hamkuambiwa tokea mwanzo? Hamkufahamu tangu kuwekwa misingi ya dunia?
22. Yeye ndiye anayeketi juu ya duara ya dunia, na hao wanaokaa ndani yake huwa kama panzi; yeye ndiye azitandazaye mbingu kama pazia na kuzikunjua kama hema ya kukaliwa;
23. ndiye awatanguaye wakuu, na kuwabatilisha waamuzi wa dunia.