Amu. 20:31-37 Swahili Union Version (SUV)

31. Nao wana wa Benyamini wakatoka waende kupigana nao, wakavutwa waende mbali na huo mji; kisha wakaanza kupiga na kuua katika hao watu, wapata kama watu thelathini wa Israeli, kama walivyofanya nyakati nyingine, katika hizo njia kuu, ambazo njia mojawapo huendelea Betheli, na njia ya pili huendelea Gibea, katika shamba.

32. Wana wa Benyamini wakasema, Wamepigwa mbele yetu kama kwanza. Lakini wana wa Israeli wakasema, Haya, na tukimbie, na kuwavuta wauache mji waende katika njia kuu.

33. Basi hao watu wote wa Israeli wakaondoka mahali pao wakajipanga huko Baal-tamari; na hao wenye kuvizia wa Israeli wakatoka mahali hapo walipokuwa, hata Maare-geba.

34. Kisha watu elfu kumi waliochaguliwa katika Israeli wote wakaja juu ya Gibea, na vile vita vilikuwa vikali sana; lakini hawakujua ya kuwa uovu ulikuwa karibu nao.

35. BWANA akampiga Benyamini mbele ya Israeli; na wana wa Israeli waliangamiza watu waume ishirini na tano elfu na mia moja, wa Benyamini siku hiyo; wote hao waliokuwa wenye kutumia upanga.

36. Basi wana wa Benyamini waliona kuwa wamepigwa; kwa kuwa watu wa Israeli wakaondoka mbele ya Benyamini, kwa sababu walikuwa wanawatumaini hao wenye kuvizia waliokuwa wamewaweka kinyume cha Gibea.

37. Hao wenye kuvizia wakafanya haraka, wakaurukia Gibea; na hao wenye kuvizia wakaenda wakaupiga huo mji wote kwa makali ya upanga.

Amu. 20