15. Basi Ishboshethi akatuma watu, akamnyang’anya Paltieli, mwana wa Laishi, mumewe, mwanamke huyo.
16. Huyo mumewe akafuatana naye, akiendelea na kulia, akamfuata mpaka Bahurimu. Ndipo Abneri akamwambia, Haya, rudi. Naye akarudi.
17. Basi Abneri akafanya mashauri na wazee wa Israeli, akasema, Zamani mlitaka Daudi awamiliki;
18. basi, sasa, fanyeni hayo; kwa maana BWANA amemtaja Daudi, akisema, kwa mkono wa mtumishi wangu, Daudi, nitawaokoa watu wangu Israeli katika mikono ya Wafilisti, na katika mikono ya adui zao wote.
19. Tena Abneri alinena masikioni mwa Benyamini; kisha Abneri akaenda ili kunena masikioni mwa Daudi huko Hebroni maneno yote yaliyoonekana kuwa mema machoni pa Israeli, na machoni pa nyumba yote ya Benyamini.
20. Basi Abneri akamwendea Daudi huko Hebroni, na watu ishirini pamoja naye. Daudi akamfanyia karamu Abneri, na watu wote waliokuwa pamoja naye.
21. Kisha Abneri akamwambia Daudi, Nitaondoka, niende zangu; nami nitamkusanyia bwana wangu mfalme Israeli wote, ili wafanye agano nawe, ukamiliki juu ya wote inaowatamani roho yako. Basi Daudi akamruhusu Abneri; naye akaenda zake kwa amani.
22. Na tazama, watumishi wa Daudi pamoja na Yoabu walitoka jeshini, wakaleta mateka mengi pamoja nao; lakini Abneri hakuwako Hebroni kwa Daudi; maana alikuwa amemruhusu, naye amekwisha kwenda zake kwa amani.
23. Hata Yoabu, na jeshi lote waliokuwa pamoja naye, walipofika, watu wakamwambia Yoabu, wakisema, Abneri, mwana wa Neri, alikuja kwa mfalme, naye amemruhusu, naye amekwenda zake kwa amani.
24. Basi Yoabu akamwendea mfalme, akasema, Umefanyaje? Tazama, Abneri amekuja kwako; mbona umemruhusu, naye amekwisha kwenda zake?
25. Wewe wamjua Abneri, mwana wa Neri, ya kuwa alikuja ili kukudanganya, apate kujua kutoka kwako, na kuingia kwako, akajue yote uyatendayo.
26. Naye Yoabu alipotoka kwa Daudi, akapeleka wajumbe kumfuata Abneri, wakamrudisha kutoka kisima cha Sira; lakini Daudi alikuwa hana habari.