2 Sam. 23:3-16 Swahili Union Version (SUV)

3. Mungu wa Israeli alisema,Mwamba wa Israeli aliniambia,Atawalaye wanadamu kwa haki,Akitawala katika kicho cha Mungu,

4. Atakuwa kama nuru ya asubuhi jua lichapo,Asubuhi isiyo na mawingu.Lachipuza majani mabichi juu ya nchi,Kwa mwangaza baada ya mvua;

5. Je! Sivyo ilivyo nyumba yangu mbele za BWANA?Kwa kuwa amefanya nami agano la milele;Ina taratibu katika yote, ni thabiti,Maana ni wokovu wangu wote, na shauku langu lote.

6. Lakini hatawachipuza watu wa ubatili;Watakuwa wote kama miiba ya nyikani ya kutupwa,Ambayo haivuniki kwa mkono,

7. Mtu atakayeigusa hiyo,Na awe na chuma na mpini wa mkuki,Nao watateketezwa papo hapo kwa moto.

8. Haya ndiyo majina ya mashujaa aliokuwa nao Daudi; Yashobeamu Mhakmoni, mkuu wa maakida; huyo aliliinua shoka lake juu ya watu mia nane waliouawa pamoja.

9. Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu waliokuwa pamoja na Daudi; walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko ili kupigana, na watu wa Israeli walikuwa wamekwenda zao;

10. huyo aliinuka, akawapiga Wafilisti hata mkono wake ukachoka, na mkono wake ukaambatana na upanga; naye BWANA akafanya wokovu mkuu siku ile; nao watu wakarudi nyuma yake ili kuteka nyara tu.

11. Na baada yake kulikuwa na Shama, mwana wa Agee, Mharari; nao Wafilisti walikuwa wamekusanyika huko Lehi, palipokuwapo konde lililojaa midengu; nao watu wakawakimbia Wafilisti;

12. ila huyo alisimama katikati ya konde lile, akalipigania, akawaua Wafilisti; naye BWANA akafanya wokovu mkuu.

13. Tena, watatu miongoni mwa wale thelathini waliokuwa wakuu wakashuka, wakamwendea Daudi wakati wa mavuno mpaka pango la Adulamu, na kikosi cha Wafilisti walikuwa wamefanya kambi katika bonde la Warefai.

14. Naye Daudi wakati ule alikuwako ngomeni, na jeshi la Wafilisti wakati ule walikuwako Bethlehemu.

15. Daudi akatamani, akasema, Laiti mtu angeninywesha maji ya kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango!

16. Basi hao mashujaa watatu wakapenya jeshi la Wafilisti, wakateka maji kutoka kile kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango, wakayachukua, wakamletea Daudi; walakini yeye hakukubali kuyanywa, akayamimina mbele za BWANA.

2 Sam. 23