2 Sam. 17:4-18 Swahili Union Version (SUV)

4. Shauri hili likawa jema machoni pa Absalomu, na machoni pa wazee wote wa Israeli.

5. Ndipo Absalomu akasema, Basi, mwiteni Hushai, Mwarki, naye, tukasikie atakayosema yeye pia.

6. Basi Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu akamwambia, akasema, Ahithofeli amesema hivi; je! Tufanye kama alivyosema? Kama sivyo, sema maneno yako.

7. Hushai akamwambia Absalomu, Shauri hili alilolitoa Ahithofeli si jema wakati huu.

8. Hushai akafuliza kusema, Wamjua baba yako na watu wake, ya kuwa ni watu mashujaa hawa, nao wana uchungu katika mioyo yao, kama dubu aliyenyang’anywa watoto wake nyikani; tena baba yako ni mtu wa vita, hatalala pamoja na watu wake.

9. Angalia, amefichwa sasa katika shimo, au penginepo; kisha itakuwa, watakapoanguka baadhi yao mwanzo, kila mtu atakayesikia, atasema, Kuna machinjo katika watu wanaofuatana na Absalomu.

10. Basi hata yeye aliye shujaa, mwenye moyo kama moyo wa simba, atayeyuka kabisa; maana Israeli wote wanajua ya kuwa baba yako ni shujaa, na ya kuwa watu wale walio pamoja naye ni mashujaa.

11. Kwa hiyo shauri langu ni hili, Waisraeli wote toka Dani mpaka Beer-sheba wakusanyike kwako, kama mchanga wa bahari kwa wingi; na wewe uende vitani mwenyewe.

12. Hivyo tutamfikia mahali po pote atakapoonekana, na kumwangukia kama vile umande uangukavyo juu ya nchi; wala hatutaacha hata mmoja wao, yeye na watu wote walio pamoja naye.

13. Tena, ikiwa amejitia katika mji uwao wote, basi Israeli wote wataleta kamba, na kuuendea mji ule, nasi tutaukokota mpaka mtoni, wala halitaonekana huko hata jiwe dogo moja la mawe yake.

14. Naye Absalomu na watu wote wa Israeli wakasema, Shauri la Hushai, Mwarki, ni jema kuliko shauri la Ahithofeli. Kwa maana BWANA alikuwa amekusudia kulivunja shauri jema la Ahithofeli, ili BWANA alete mabaya juu ya Absalomu.

15. Ndipo Hushai akawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani, Ahithofeli amempa Absalomu na wazee wa Israeli mashauri kadha wa kadha; na mimi nimetoa mashauri kadha wa kadha.

16. Basi sasa pelekeni habari upesi kamwambieni Daudi ya kwamba, Usilale usiku huu karibu na vivuko vya jangwani; bali usikose kuvuka; asije akamezwa mfalme, na watu wote walio pamoja naye.

17. Basi Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakikaa karibu na Enrogeli; na mjakazi mmoja alikuwa akienda na kuwapa habari; nao huenda kumwambia mfalme Daudi; maana ilikuwa lazima wasionekane wakiingia mjini.

18. Lakini kijana mmoja aliwaona, akamwambia Absalomu; basi wakaenda wote wawili kwa haraka, wakafika Bahurimu, nyumbani kwa mtu aliyekuwa na kisima uani mwake; wakashuka ndani yake.

2 Sam. 17