14. akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni, wala duniani; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa moyo wao wote;
15. uliyemtimizia mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidi; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo.
16. Sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, umfikilizie mtumishi wako Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu machoni pangu, wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli; wakiwa tu watoto wako wataiangalia njia yao, ili kuiendea torati yangu, kama wewe ulivyokwenda mbele zangu.
17. Basi sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako Daudi.
18. Lakini Mungu je! Yamkini atakaa na watu duniani? Tazama, mbingu na mbingu za mbingu za mbingu hazikutoshi; siuze nyumba hii niliyoijenga!
19. Walakini umwangalie mtumwa wako anayoyaomba, na kusihi, Ee BWANA, Mungu wangu, usikie kilio na maombi anayoyaomba mtumwa wako mbele zako;
20. ili macho yako yafumbuke kwa nyumba hii mchana na usiku, mahali uliponena, ndipo utakapoliweka jina lako; usikie maombi atakayoomba mtumwa wako, akikabili mahali hapa.
21. Uyasikie atakayosihi mtumwa wako, na watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, usikie toka makaoni mwako, toka mbinguni, nawe usikiapo, samehe.
22. Ikiwa mtu amemkosea mwenzake, akitiwa kiapo, aapishwe, naye akija na kuapa hapa mbele ya madhabahu yako nyumbani humu;
23. basi, usikie mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumwa wako; ukimlipiza mwovu, kumpatilizia njia yake kichwani; ukamfanyie haki mwenye haki, ukimjalia kwa kadiri ya haki yake.
24. Ikiwa watu wako Israeli wamepigwa mbele ya adui zao, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakirejea kwako, na kulikiri jina lako, wakikuomba na kukusihi nyumbani humu;
25. basi usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watu wako Israeli, na kuwarejeza tena katika nchi uliyowapa wao na baba zao.
26. Ikiwa mbingu zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakiomba wakikabili mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kuiacha dhambi yao, uwatesapo;
27. basi usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watumwa wako, na ya watu wako Israeli; uwafundishapo njia njema iwapasayo waiendee; ukainyeshee mvua nchi yako, uliyowapa watu wako iwe urithi.
28. Ikiwa nchi imeingia njaa, au tauni, au ukosefu wa mvua, au ukungu, au nzige, au panzi; ikiwa adui wamewahusuru katika nchi ya miji yao, au ukiwapo msiba wo wote, au uele wo wote;
29. yo yote atakayoyaomba na kusihi mtu awaye yote, au watu wako Israeli wote pamoja, watakaojua kila mtu pigo lake mwenyewe, na msiba wake mwenyewe, akiinyoshea mikono nyumba hii;
30. basi usikie huko mbinguni, ukaapo, ukasamehe, ukampatilize kila mtu kwa kadiri ya njia zake zote; wewe umjuaye moyo; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu);