15. Kisha wakaichinja pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili, nao makuhani na Walawi wakatahayarika, wakajitakasa, wakaleta sadaka za kuteketezwa nyumbani mwa BWANA.
16. Wakasimama mahali pao kwa taratibu yao, sawasawa na torati ya Musa, mtu wa Mungu; nao makuhani wakainyunyiza damu, waliyoipokea mikononi mwa Walawi.
17. Kwa maana kulikuwa na wengi katika kusanyiko ambao hawajajitakasa; kwa hiyo Walawi wakamchinjia pasaka, kila mtu asiyekuwa safi, ili kuwatakasa kwa BWANA.
18. Kwani wingi wa watu, naam, wengi wa Efraimu, na wa Manase, na wa Isakari, na wa Zabuloni, hawakujisafisha, lakini wakala pasaka, ila si kama ilivyoandikwa. Naye Hezekia alikuwa amewaombea, akisema, BWANA mwema na amsamehe kila mtu,
19. aukazaye moyo wake kumtafuta Mungu, BWANA, Mungu wa babaze, hata ikiwa si kwa utakaso wa patakatifu.
20. BWANA akamsikia Hezekia, akawaponya watu.
21. Nao wana wa Israeli waliohudhuria Yerusalemu wakafanya sikukuu ya mikate isiyochachwa siku saba kwa furaha kubwa; Walawi na makuhani wakamsifu BWANA siku kwa siku, wakimwimbia BWANA kwa vinanda vyenye sauti kuu.
22. Hezekia akawafurahisha mioyo Walawi wote waliokuwa wastadi wa kumtumikia BWANA. Basi muda wa siku saba wakala sikukuu, wakitoa dhabihu za sadaka za amani, na kumtolea shukrani BWANA, Mungu wa baba zao.
23. Na kusanyiko lote wakafanya shauri kufanya sikukuu siku saba nyingine; wakafanya sikukuu siku saba nyingine kwa furaha.