2 Nya. 30:10-22 Swahili Union Version (SUV)

10. Basi matarishi wakapita mji kwa mji kati ya nchi ya Efraimu na Manase, hata kufika Zabuloni; lakini waliwacheka-cheka, na kuwadhihaki.

11. Ila watu wengine wa Asheri, na wa Manase, na wa Zabuloni walijinyenyekeza, wakaja Yerusalemu.

12. Tena katika Yuda mkono wa Mungu ulikuwa ukiwapa moyo mmoja, waitimize amri ya mfalme na wakuu kwa neno la BWANA.

13. Basi wakakusanyika Yerusalemu watu wengi ili kuifanya sikukuu ya mikate isiyochachwa katika mwezi wa pili, kusanyiko kuu sana.

14. Wakainuka, wakaziondoa madhabahu zilizokuwamo Yerusalemu, nazo madhabahu za kufukizia wakaziondoa, wakazitupa katika kijito Kidroni.

15. Kisha wakaichinja pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili, nao makuhani na Walawi wakatahayarika, wakajitakasa, wakaleta sadaka za kuteketezwa nyumbani mwa BWANA.

16. Wakasimama mahali pao kwa taratibu yao, sawasawa na torati ya Musa, mtu wa Mungu; nao makuhani wakainyunyiza damu, waliyoipokea mikononi mwa Walawi.

17. Kwa maana kulikuwa na wengi katika kusanyiko ambao hawajajitakasa; kwa hiyo Walawi wakamchinjia pasaka, kila mtu asiyekuwa safi, ili kuwatakasa kwa BWANA.

18. Kwani wingi wa watu, naam, wengi wa Efraimu, na wa Manase, na wa Isakari, na wa Zabuloni, hawakujisafisha, lakini wakala pasaka, ila si kama ilivyoandikwa. Naye Hezekia alikuwa amewaombea, akisema, BWANA mwema na amsamehe kila mtu,

19. aukazaye moyo wake kumtafuta Mungu, BWANA, Mungu wa babaze, hata ikiwa si kwa utakaso wa patakatifu.

20. BWANA akamsikia Hezekia, akawaponya watu.

21. Nao wana wa Israeli waliohudhuria Yerusalemu wakafanya sikukuu ya mikate isiyochachwa siku saba kwa furaha kubwa; Walawi na makuhani wakamsifu BWANA siku kwa siku, wakimwimbia BWANA kwa vinanda vyenye sauti kuu.

22. Hezekia akawafurahisha mioyo Walawi wote waliokuwa wastadi wa kumtumikia BWANA. Basi muda wa siku saba wakala sikukuu, wakitoa dhabihu za sadaka za amani, na kumtolea shukrani BWANA, Mungu wa baba zao.

2 Nya. 30