1. Hata mwaka wa saba Yehoyada akajitia nguvu, akawatwaa maakida wa mamia, Azaria mwana wa Yerohamu, na Ishmaeli mwana wa Yehohanani, na Azaria mwana wa Obedi, na Maaseya mwana wa Adaya, na Elishafati mwana wa Zikri, akapatana nao.
2. Wakazunguka katikati ya Yuda, wakawakusanya Walawi kutoka katika miji yote ya Yuda, na wakuu wa nyumba za mababa wa Israeli, wakaja Yerusalemu.
3. Na kusanyiko lote wakafanya agano na mfalme nyumbani mwa Mungu. Akawaambia, Angalieni, mwana wa mfalme atatawala, kama BWANA alivyonena juu ya wana wa Daudi.
4. Hili ndilo neno mtakalolifanya; theluthi yenu, ninyi mwingiao siku ya sabato, wa makuhani, na wa Walawi, mtalinda milangoni;
5. na theluthi nyumbani pa mfalme; na theluthi mlangoni pa msingi; na watu wote watakuwapo nyuani mwa nyumba ya BWANA.
6. Wala asiingie mtu nyumbani mwa BWANA, ila makuhani, na hao watumikao wa Walawi; hao wataingia, kwa kuwa hao ni watakatifu; ila watu wote watalinda malinzi ya BWANA.
7. Nao Walawi watamzunguka mfalme pande zote, kila mtu mwenye silaha zake mkononi; naye awaye yote aingiaye nyumbani na auawe; nanyi mfuatane na mfalme, aingiapo na atokapo.
8. Basi Walawi na Yuda wote wakafanya sawasawa na yote aliyowaamuru Yehoyada kuhani; wakawatwaa kila mtu watu wake, hao watakaoingia siku ya sabato, na wale watakaotoka siku ya sabato; kwa maana Yehoyada kuhani hakuzifumua zamu.
9. Naye Yehoyada kuhani akawapa maakida wa mamia mikuki, na ngao, na vigao, vilivyokuwa vya mfalme Daudi, vilivyokuwamo nyumbani mwa Mungu.
10. Akawasimamisha watu wote, kila mtu mwenye silaha yake mkononi, toka pembe ya kuume ya nyumba mpaka pembe ya kushoto, upande wa madhabahu na nyumba, kumzunguka mfalme pande zote.
11. Ndipo wakamleta nje mwana wa mfalme, wakamvika taji, na kumpa ule ushuhuda, wakamtawaza awe mfalme; Yehoyada na wanawe wakamtia mafuta, wakasema, Mfalme na aishi.
12. Na Athalia alipoisikia sauti ya watu, na ya walinzi, na ya hao waliomsifu mfalme, akaingia kwa watu nyumbani mwa BWANA;