2 Fal. 18:1-12 Swahili Union Version (SUV)

1. Ikawa katika mwaka wa tatu wa Hoshea, mwana wa Ela, mfalme wa Israeli, Hezekia, mwana wa Ahazi, mfalme wa Yuda, alianza kutawala.

2. Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na kenda katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Abiya, binti Zekaria.

3. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, mfano wa yote aliyoyafanya Daudi, baba yake.

4. Alipaondoa mahali pa juu, akazibomoa nguzo, akaikata hiyo Ashera; akaivunja vipande vipande ile nyoka ya shaba aliyoifanya Musa; maana hata siku zile wana wa Israeli walikuwa wakiifukizia uvumba; naye akaiita jina lake Nehushtani.

5. Alimtumaini BWANA, Mungu wa Israeli; hata baada yake hapakuwa na mfano wake katika wafalme wote wa Yuda, wala katika hao waliomtangulia.

6. Maana alishikamana na BWANA, hakuacha kumfuata, bali alizishika amri zake BWANA alizomwamuru Musa.

7. Naye BWANA akawa pamoja naye, kila alikokwenda alifanikiwa; tena alimwasi mfalme wa Ashuru, wala hakumtumikia.

8. Akawapiga Wafilisti mpaka Gaza na mipaka yake, tangu mnara wa walinzi hata mji wenye boma.

9. Hata katika mwaka wa nne wa Hezekia, ndio mwaka wa saba wa Hoshea, mwana wa Ela, mfalme wa Israeli, Shalmanesa, mfalme wa Ashuru, akakwea ili kupigana na Samaria, akauhusuru.

10. Wakautwaa baada ya miaka mitatu; yaani, katika mwaka wa sita wa Hezekia, ndio mwaka wa kenda wa Hoshea, mfalme wa Israeli, ndipo Samaria ulipotwaliwa.

11. Mfalme wa Ashuru akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala, na katika Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi;

12. kwa sababu hawakuitii sauti ya BWANA, Mungu wao, bali waliyahalifu maagano yake, mambo yote ambayo Musa mtumishi wa BWANA aliwaamuru, wasikubali kuyasikiliza, wala kuyatenda.

2 Fal. 18