12. Basi Mikali akamtelemsha Daudi dirishani; naye akaenda akakimbia na kuokoka.
13. Ndipo Mikali akakitwaa kinyago, na kukilaza kitandani, akatia na mto wa singa za mbuzi kichwani pake, na kukifunika kwa nguo.
14. Naye Sauli alipotuma wajumbe ili kumkamata Daudi, yeye alisema, Hawezi.
15. Basi Sauli akawatuma hao wajumbe ili wamtazame Daudi, akisema, Mleteni kwangu juu ya kitanda chake, nipate kumwua.
16. Nao wajumbe walipoingia, kumbe! Kuna kinyago kitandani, na mto wa singa za mbuzi kichwani pake!
17. Sauli akamwambia Mikali, Mbona wewe umenidanganya hivi, na kumwacha adui yangu aende, hata ameniponyoka? Naye Mikali akamjibu Sauli, Yeye aliniambia, Niache niende zangu; kwa nini nikuue?
18. Hivyo Daudi akakimbia, akajiponya, akamwendea Samweli huko Rama, akamwambia hayo yote Sauli aliyomtenda. Kisha yeye na Samweli wakaenda na kukaa katika Nayothi.
19. Naye Sauli akaambiwa, kusema, Angalia, yule Daudi yuko katika Nayothi, huko Rama.
20. Basi Sauli akatuma wajumbe ili kumkamata Daudi; nao hapo walipowaona jamaa ya manabii wakitabiri, na Samweli amesimama kama mkuu wao, roho ya Mungu ikawajilia wajumbe wa Sauli, nao pia wakatabiri.
21. Naye Sauli alipoambiwa, alituma wajumbe wengine, wao nao wakatabiri. Naye Sauli akatuma wajumbe tena mara ya tatu, na wao pia wakatabiri.
22. Kisha yeye mwenyewe akaenda Rama, akafika kunako kile kisima kikubwa kilicho huko Seku; akauliza, akasema, Je! Wako wapi Samweli na Daudi? Na mtu mmoja akajibu, Tazama, wako Nayothi, huko Rama.
23. Basi akaenda Nayothi huko Rama, na roho ya Mungu ikamjilia yeye naye, akaendelea mbele, huku anatabiri, mpaka kufika Nayothi huko Rama.