1 Sam. 16:4-19 Swahili Union Version (SUV)

4. Samweli akafanya hayo aliyosema BWANA, akaenda Bethlehemu. Wakaja wazee wa mji kumlaki, wakitetemeka, nao wakasema, Je! Umekuja kwa amani?

5. Naye akasema, Naam, kwa amani; nimekuja kumtolea BWANA dhabihu; jitakaseni; njoni pamoja nami kwenye dhabihu. Akawatakasa Yese na wanawe, akawaita kwenye dhabihu.

6. Ikawa walipokuja, alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake.

7. Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo.

8. Ndipo Yese akamwita Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, BWANA hakumchagua huyu.

9. Ndipo Yese akampitisha Shama. Naye akasema, wala BWANA hakumchagua huyu.

10. Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, BWANA hakuwachagua hawa.

11. Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku.

12. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. BWANA akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye.

13. Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya BWANA ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.

14. Basi, roho ya BWANA ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa BWANA ikamsumbua.

15. Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua.

16. Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujilia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona.

17. Basi Sauli akawaambia, Vema, nitafutieni mtu aliye stadi wa kupiga kinubi, mkaniletee.

18. Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye BWANA yu pamoja naye.

19. Basi Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee Daudi mwanao, aliye pamoja na kondoo.

1 Sam. 16