1 Sam. 15:19-32 Swahili Union Version (SUV)

19. Mbona, basi, hukuitii sauti ya BWANA, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA?

20. Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya BWANA, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa.

21. Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng’ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa BWANA, Mungu wako, huko Gilgali.

22. Naye Samweli akasema,je! BWANA huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihuSawasawa na kuitii sauti ya BWANA?Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu,Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.

23. Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi,Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago;Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA,Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.

24. Ndipo Sauli akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya BWANA, pia na maneno yako; kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao.

25. Basi sasa, nakuomba, unisamehe dhambi yangu; rudi pamoja nami, nipate kumwabudu BWANA.

26. Samweli akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la BWANA, BWANA naye amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli.

27. Naye Samweli alipogeuka, aende zake, Sauli akaushika upindo wa vazi lake, nalo likararuka.

28. Basi Samweli akamwambia, Leo BWANA amekurarulia ufalme wa Israeli, naye amempa jirani yako, aliye mwema kuliko wewe.

29. Tena Yeye aliye Nguvu za Israeli hatanena uongo, wala hataona majuto; maana siye mwanadamu, hata ajute.

30. Akasema, Nimekosa; lakini uniheshimu sasa, nakuomba, mbele ya wazee wa watu wangu, na mbele ya Israeli, rudi pamoja nami, nimwabudu BWANA, Mungu wako.

31. Basi Samweli akarudi na kuandamana na Sauli; naye Sauli akamwabudu BWANA.

32. Ndipo Samweli akasema, Nileteeni hapa Agagi, mfalme wa Waamaleki. Basi Agagi akamwendea kwa utepetevu. Naye Agagi akasema, Bila shaka uchungu wa mauti umeondoka.

1 Sam. 15