6. Makuhani wakalileta sanduku la agano la BWANA hata mahali pake, katika chumba cha ndani cha ile nyumba, patakatifu pa patakatifu, naam, chini ya mbawa za makerubi.
7. Kwa maana makerubi yalinyosha mbawa zao, juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu.
8. Na ile miti kwa kuwa mirefu, ncha za miti zilionekana katika mahali patakatifu, mbele ya chumba cha ndani; lakini hazikuonekana nje; nayo iko kuko huko hata leo.
9. Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliziweka ndani huko Horebu, BWANA alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka katika nchi ya Misri.
10. Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya BWANA ikajaa wingu;
11. hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya BWANA ilikuwa imejaa utukufu wa BWANA.
12. Ndipo Sulemani akanena, BWANA alisema ya kwamba atakaa katika giza nene.
13. Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele.
14. Mfalme akageuza uso wake, akawabariki mkutano wote wa Israeli; na mkutano wote wa Israeli wakasimama.
15. Akasema, BWANA, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenena na Daudi baba yangu kwa kinywa chake akalitimiza kwa mkono wake, akasema,
16. Tokea siku ile nilipowatoa watu wangu Israeli katika Misri, sikuchagua mji wo wote katika kabila zote za Israeli ili kujenga nyumba, jina langu liwe hapo; lakini nalimchagua Daudi awe juu ya watu wangu Israeli.
17. Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli.