7. Ndipo mfalme wa Israeli, akawaita wazee wote wa nchi, akasema, Angalieni, nawaomba, mwone, kwamba huyu ataka madhara; maana ametuma kwangu kutaka wake zangu na watoto wangu; na fedha yangu na dhahabu yangu, sikumkatalia.
8. Wakamwambia wazee wote na watu wote, Usisikie, wala usikubali.
9. Kwa hiyo akawaambia wale wajumbe wa Ben-hadadi, Mwambieni bwana wangu mfalme, Kila uliyotuma kumtakia mtumwa wako kwanza, nitafanya, ila neno hili siwezi kulifanya. Basi wajumbe wakaenda zao, wakamrudishia maneno hayo.
10. Ndipo Ben-hadadi akatuma kwake, akasema, Miungu wanifanyie hivi na kuzidi, yakiwa mavumbi ya Samaria yatatosha makonzi ya watu wote walio miguuni pangu.
11. Mfalme wa Israeli akajibu, akasema, Mwambieni, Avaaye asijisifu kama avuaye.
12. Ikawa, Ben-hadadi alipolisikia neno hilo, naye alikuwa akinywa, yeye na wafalme, mabandani, aliwaambia watumwa wake, Jipangeni. Wakajipanga juu ya mji.
13. Na tazama, nabii akamjia Ahabu mfalme wa Israeli, akasema, BWANA asema hivi, Je! Umeona makutano haya yote walio wengi? Angalia, nitawatia leo mkononi mwako; nawe utajua ya kuwa ndimi BWANA.
14. Ahabu akanena, Kwa nani? Akasema, BWANA asema hivi, Kwa vijana wa maliwali wa majimbo. Ndipo akanena, Ni nani atakayepanga vita? Naye akajibu, Ni wewe.
15. Ndipo akawaandika vijana wa maliwali wa majimbo, nao walikuwa mia mbili thelathini na wawili; kisha baada ya hao akawaandika watu wote, wana wa Israeli wote, nao walikuwa elfu saba.
16. Wakatoka wakati wa adhuhuri. Lakini Ben-hadadi alikuwa akinywa hata kulewa mabandani, yeye na wale wafalme thelathini na wawili waliomsaidia.
17. Wakatoka wale vijana wa maliwali wa majimbo wakitangulia; na Ben-hadadi akatuma watu, nao wakamwambia, Wako watu wametoka katika Samaria.
18. Akasema, Kwamba wametoka kwa amani, wakamateni wa hai; au kwamba wametoka kwa vita, wakamateni wa hai.
19. Basi wakatoka mjini hao vijana wa maliwali wa majimbo, na jeshi nyuma yao.
20. Wakapiga kila mmoja mtu wake; Washami wakakimbia, na Israeli wakawafuatia; Ben-hadadi mfalme wa Shamu akaokoka amepanda farasi, pamoja na wapandao farasi.
21. Mfalme wa Israeli akatoka, akawapiga farasi na magari, akawapiga Washami pigo kubwa.
22. Naye yule nabii akamjia mfalme wa Israeli, akamwambia, Enenda, kusanya nguvu zako, ujue, na kuangalia ufanyavyo; kwa maana mwakani mfalme wa Shamu atakuja juu yako.
23. Basi watumwa wake mfalme wa Shamu wakamwambia, Mungu wao ni mungu wa milima; ndiyo sababu ya kutushinda sisi; lakini na tupigane nao katika nchi tambarare, na hakika tutawashinda wao.
24. Ufanye neno hili; uwaondoe hao wafalme, kila mtu atoke mahali pake, ukaweke majemadari mahali pao.
25. Kisha ujihesabie jeshi, kama jeshi lililokupotea, farasi kwa farasi na gari kwa gari; nasi tutapigana nao katika nchi tambarare, na bila shaka tutawashinda. Akaisikiliza sauti yao, akafanya kama hivyo.