1 Fal. 16:7-18 Swahili Union Version (SUV)

7. Tena neno la BWANA likaja kwa mkono wa nabii Yehu mwana wa Hanani juu ya Baasha, na juu ya nyumba yake, kwa sababu ya mabaya yote aliyoyatenda machoni pa BWANA, akimghadhibisha kwa kazi ya mikono yake, kwa kufanana na nyumba ya Yeroboamu, na kwa sababu aliiharibu.

8. Katika mwaka wa ishirini na sita wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha alianza kutawala juu ya Israeli huko Tirza, akatawala miaka miwili.

9. Na mtumwa wake Zimri, jemadari wa nusu ya magari yake, akamfanyia fitina; alipokuwako Tirza akinywa hata kulewa nyumbani mwa Arsa, aliyekuwa juu ya nyumba huko Tirza;

10. Zimri akaingia akampiga, akamwua, katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, akatawala mahali pake.

11. Ikawa, alipoanza kutawala, mara alipoketi juu ya kiti chake cha enzi, akawaua nyumba yote ya Baasha; hakumwachia mwanamume ye yote, wa jamaa zake, wala wa rafiki zake.

12. Hivyo Zimri akaiharibu nyumba yote ya Baasha, sawasawa na neno la BWANA, alilolinena juu ya Baasha kwa Yehu nabii,

13. kwa sababu ya makosa yake Baasha, na makosa yote ya Ela mwanawe, waliyoyakosa, na kuwakosesha Israeli, wakimghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kwa matendo yao ya ubatili.

14. Na mambo yote ya Ela yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?

15. Katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala muda wa siku saba huko Tirza. Basi, watu walikuwa wametua maragoni kupigana na Gibethoni, ulio wa Wafilisti.

16. Na hao watu waliokuwako maragoni wakasikia habari ya kwamba Zimri amefanya fitina, tena amempiga mfalme; kwa hiyo Israeli wote wakamfanya Omri, jemadari wa jeshi, awe mfalme juu ya Israeli siku ile maragoni.

17. Omri akapanda kutoka Gibethoni, na Israeli wote pamoja naye, wakauhusuru Tirza.

18. Ikawa Zimri alipoona ya kuwa mji umetwaliwa, akaingia ngomeni mwa nyumba ya mfalme, akaiteketeza nyumba ya mfalme juu yake kwa moto, akafa;

1 Fal. 16