23. Tena, Mungu akamwondokeshea adui mwingine, Rezoni mwana wa Eliada, aliyemkimbia bwana wake Hadadezeri mfalme wa Soba,
24. naye akakusanya watu, akawa mkuu wa jeshi, hapo Daudi alipowaua hao watu wa Soba; wakaenda Dameski, wakakaa humo, na kumiliki huko Dameski.
25. Naye akawa adui wa Israeli siku zote za Sulemani, zaidi ya madhara yake Hadadi; naye akawachukia Israeli, akamiliki juu ya Shamu.
26. Na Yeroboamu wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumwa wake Sulemani; ambaye jina lake mamaye aliitwa Serua, mwanamke aliyefiwa na mumewe; yeye naye akainua mkono wake juu ya mfalme.
27. Na hii ndiyo sababu ya yeye kumwinulia mfalme mkono. Sulemani aliijenga Milo, akapafunga palipobomoka pa mji wa baba yake Daudi.
28. Na huyo Yeroboamu alikuwa mtu hodari, shujaa; Sulemani akaona ya kuwa kijana huyo ni mtu mwenye bidii, akamweka juu ya kazi yote ya nyumba ya Yusufu.
29. Ikawa zamani zile Yeroboamu alipokuwa akitoka katika Yerusalemu, nabii Ahiya, Mshiloni, alikutana naye njiani; naye Ahiya amevaa vazi jipya, na hao wawili walikuwa peke yao mashambani.
30. Ahiya akalishika lile vazi jipya alilokuwa amelivaa, akalirarua vipande kumi na viwili.
31. Akamwambia Yeroboamu, Twaa wewe vipande kumi, maana BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika mkono wa Sulemani, nami nitakupa wewe kabila kumi,
32. (lakini yeye atakuwa na kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya Yerusalemu mji ule niliouchagua katika miji yote ya kabila za Israeli);
33. kwa sababu wameniacha mimi wakaabudu Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni, na Kemoshi, mungu wa Wamoabi, na Milkomu, mungu wa wana wa Amoni wala hawakuenda katika njia zangu, kutenda mema machoni pangu, kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, kama Daudi baba yake.
34. Walakini sitauondoa ufalme wote katika mkono wake; lakini nitamfanya awe mkuu siku zote za maisha yake, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi niliyemchagua kwa maana alizishika amri zangu na sheria zangu,
35. lakini nitauondoa ufalme katika mkono wa mwanawe, nami nitakupa wewe kabila kumi.
36. Nami nitampa mwana wake kabila moja, ili Daudi, mtumishi wangu, apate kuwa na taa siku zote mbele zangu katika Yerusalemu, mji ule niliouchagua niweke jina langu huko.