1. Mfalme Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao wakamfunika nguo, lakini asipate moto.
2. Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, Bwana wangu mfalme na atafutiwe kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya mfalme, amtunze; alale kifuani mwako, ili bwana wangu mfalme apate moto.
3. Basi wakatafuta kijana mzuri mipakani mwote mwa Israeli, wakamwona Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme.
4. Naye kijana huyo alikuwa mzuri sana; akamtunza mfalme, akamtumikia; walakini mfalme hakumjua.
5. Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akatakabari, akasema, Mimi nitakuwa mfalme. Akajiwekea tayari magari na wapanda farasi, na watu hamsini wapige mbio mbele yake.
6. Tena baba yake hakumchukiza wakati wo wote kwa kusema, Mbona umefanya hivi? Kisha, alikuwa mtu mzuri sana; naye alizaliwa baada ya Absalomu.
7. Akashauriana na Yoabu, mwana wa Seruya, na Abiathari, kuhani; nao wakamsaidia Adonia, wakamfuata.
8. Ila Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Nathani, nabii, na Shimei, na Rei, na mashujaa wa Daudi, hao hawakuwa pamoja na Adonia.
9. Adonia akachinja kondoo, na ng’ombe, na vinono, karibu na jiwe la Zohelethi, lililo karibu na chemchemi Rogeli; akawaita ndugu zake wote, wana wa mfalme, na watu wote wa Yuda, watumishi wa mfalme;
10. ila Nathani, nabii, na Benaya, na mashujaa, na Sulemani nduguye, hakuwaita hao.
11. Ndipo Nathani akamwambia Bath-sheba, mamaye Sulemani, akasema, Je! Hukusikia ya kuwa Adonia, mwana wa Hagithi, anamiliki, na bwana wetu Daudi hana habari?
12. Haya basi, nikupe shauri, tafadhali, upate kuiokoa roho yako, na roho ya mwanao Sulemani.
13. Enenda uingie ndani kwa mfalme Daudi, ukamwambie, Je! Hukuniapia mimi mjakazi wako, Ee mfalme, bwana wangu, kusema, Hakika yake Sulemani mwana wako atamiliki baada yangu, na kuketi katika kiti changu cha enzi? Mbona basi anamiliki Adonia?
14. Tazama, wakati ule utakapokuwa katika kusema na mfalme, mimi nami nitaingia nyuma yako, na kuyahakikisha maneno yako.
15. Basi Bath-sheba akaingia ndani kwa mfalme, ndani ya chumba chake; naye mfalme alikuwa mzee sana; na Abishagi, Mshunami, alikuwa akimtumikia mfalme.
16. Bath-sheba akainama, akamsujudia mfalme. Naye mfalme akamwuliza, Wataka nini?
17. Akamwambia, Bwana wangu, uliniapia mimi mjakazi wako kwa BWANA, Mungu wako, ya kwamba, bila shaka Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, yeye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi.