Yer. 9:12-26 Swahili Union Version (SUV)

12. Ni nani aliye na hekima, apate kuelewa na haya? Tena ni nani ambaye kinywa cha BWANA kimesema naye, apate kuyatangaza? Nayo ni nini maana yake nchi hii kuharibika, na kuteketea kama nyika, asipite mtu?

13. Naye BWANA asema, Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu niliyoweka mbele yao, wala hawakuitii sauti yangu, wala kuenenda katika hiyo;

14. bali wameenenda katika ushupavu wa mioyo yao wenyewe, na kuandamana na Mabaali, kama walivyofundishwa na baba zao.

15. Basi, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitawalisha pakanga, naam, watu hawa, nami nitawapa maji ya uchungu wayanywe.

16. Nami nitawatawanya kati ya mataifa, ambao wao hawakuwajua; wala baba zao, nami nitatuma upanga nyuma yao, hata nitakapowaangamiza kabisa.

17. BWANA wa majeshi asema hivi, Fikirini ninyi, mkawaite wanawake waombolezao, ili waje; mkatume na kuwaita wanawake wenye ustadi, ili waje;

18. na wafanye haraka na kutuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujike maji.

19. Maana sauti ya maombolezo imesikiwa toka Sayuni,Jinsi tulivyotekwa!tulivyofadhaika sana!Kwa sababu tumeiacha nchi,kwa kuwa wameangusha makao yetu.

20. Lakini lisikieni neno la BWANA, enyi wanawake,Na masikio yenu yapokee neno la kinywa chake;Mkawafundishe binti zenu kuomboleza,Na kila mmoja jirani yake kulia.

21. Kwa maana mauti imepandia madirishani mwetu,imeingia majumbani mwetu;Ipate kuwakatilia mbali watoto walio nje,na vijana katika njia kuu.

22. Nena, BWANA asema hivi,Mizoga ya watu itaangukakama samadi juu ya mashamba,Na kama konzi ya ngano nyuma yake avunaye,wala hapana mtu atakayeikusanya.

23. BWANA asema hivi, Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake;

24. bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni BWANA, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema BWANA,

25. Tazama, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapowaadhibu wote waliotahiriwa katika hali yao ya kutokutahiriwa;

26. Misri, na Yuda, na Edomu, na wana wa Amoni, na Moabu, na wote wenye kunyoa denge, wakaao nyikani; maana mataifa hayo yote hawana tohara, wala nyumba yote ya Israeli hawakutahiriwa mioyo yao.

Yer. 9