Yer. 51:53-64 Swahili Union Version (SUV)

53. Babeli ujapopanda mbinguni, na ujapopafanya mahali pa juu penye nguvu zake kuwa ngome, hata hivyo toka kwangu wenye kuangamiza watamwendea, asema BWANA.

54. Sauti ya kilio kutoka Babeli,Na ya uangamivu mkuu toka nchi ya Wakaldayo!

55. Maana BWANA amwangamiza Babeli,Na kuikomesha sauti kuu ndani yake;Na mawimbi yake yavuma kama maji mengi,Mshindo wa sauti zao wafanya makelele;

56. Kwa maana mwenye kuangamiza amefika kwake;Naam, amefika Babeli;Na mashujaa wake wametwaliwa;Pinde zao zimevunjika kabisa;Maana BWANA ni Mungu wa kisasi;Hakika yake yeye atalipa.

57. Nami nitawalevya wakuu wake, na watu wake wenye hekima, maliwali wake, na maakida wake, na mashujaa wake; nao watalala usingizi wa milele, wasiamke, asema Mfalme, BWANA wa majeshi, ambaye jina lake ni BWANA.

58. BWANA wa majeshi asema hivi, Kuta pana za Babeli zitabomolewa kabisa, na malango yake marefu yatateketezwa; nao watu watajitaabisha kwa ubatili, na mataifa kwa moto; nao watachoka.

59. Neno ambalo Yeremia, nabii, alimwamuru Seraya, mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, alipokwenda Babeli pamoja na Sedekia, mfalme wa Yuda, katika mwaka wa nne wa kumiliki kwake. Basi Seraya alikuwa msimamizi mkuu wa nyumba ya mfalme.

60. Naye Yeremia akaandika katika kitabu habari ya mabaya yote yatakayoupata Babeli, maneno hayo yote yaliyoandikwa juu ya Babeli.

61. Naye Yeremia akamwambia Seraya, Utakapofika Babeli, basi angalia uyasome maneno haya yote,

62. ukaseme, Ee BWANA, umenena habari za mji huu kwamba utakatiliwa mbali, usikaliwe na awaye yote, wala wanadamu wala wanyama, lakini uwe ukiwa hata milele.

63. Tena itakuwa utakapokwisha kukisoma kitabu hicho, utakifungia jiwe, na kukitupa katika mto Frati;

64. nawe utasema, Hivyo ndivyo utakavyozama Babeli, wala hautazuka tena, kwa sababu ya mabaya yote nitakayoleta juu yake; nao watachoka. Maneno ya Yeremia yamefika hata hapa.

Yer. 51