Yer. 31:2-20 Swahili Union Version (SUV)

2. BWANA asema hivi, Watu wale walioachwa na upanga walipata neema jangwani; yaani, Israeli, hapo nilipokwenda kumstarehesha.

3. BWANA alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu.

4. Mara ya pili nitakujenga, nawe utajengwa, Ee bikira wa Israeli mara ya pili utapambwa kwa matari yako, nawe utatokea katika michezo yao wanaofurahi.

5. Mara ya pili utapanda mizabibu juu ya milima ya Samaria; wapanzi watapanda, nao watayafurahia matunda yake.

6. Maana kutakuwa siku moja, ambayo walinzi watalia juu ya vilima vya Efraimu, Inukeni, tukaende Sayuni, kwa BWANA, Mungu wetu.

7. Maana BWANA asema hivi, Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee BWANA, uwaokoe watu wako, mabaki ya Israeli.

8. Tazama, nitawaleta toka nchi ya kaskazini, na kuwakusanya katika miisho ya dunia, na pamoja nao watakuja walio vipofu, na hao wachechemeao, mwanamke mwenye mimba, na yeye pia aliye na utungu wa kuzaa; watarudi huko, jeshi kubwa.

9. Watakuja kwa kulia, na kwa maombi nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyoka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu.

10. Lisikieni neno la BWANA, enyi mataifa, litangazeni visiwani mbali; mkaseme, Aliyemtawanya Israeli atamkusanya, na kumlinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake.

11. Kwa maana BWANA amemweka huru Yakobo, amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye.

12. Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sayuni, wataukimbilia wema wa BWANA, nafaka, na divai, na mafuta, na wachanga wa kondoo na wa ng’ombe; na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji; wala hawatahuzunika tena kabisa.

13. Ndipo bikira atafurahi katika kucheza, na vijana na wazee pamoja; maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha, nami nitawafariji, na kuwafurahisha waache huzuni zao.

14. Nami nitaishibisha roho ya makuhani kwa unono, na watu wangu watashiba kwa wema wangu, asema BWANA

15. BWANA asema hivi,Sauti imesikiwa Rama,kilio, na maombolezo mengi,Raheli akiwalilia watoto wake;asikubali kufarijiwa kwa watoto wake, kwa kuwa hawako,

16. BWANA asema hivi,Zuia sauti yako, usilie,na macho yako yasitoke machozi;Maana kazi yako itapata thawabu,nao watakuja tena toka nchi ya adui;Ndivyo asemavyo BWANA.

17. Tena liko tumaini kwa siku zako za mwisho, asema BWANA; na watoto wako watarejea hata mpaka wao wenyewe.

18. Hakika nimemsikia Efraimu, akijililia hivi, Umeniadhibu, nami nikaadhibika, kama ndama asiyeizoelea nira; unigeuze, nami nitageuzwa; kwa maana wewe u BWANA, Mungu wangu.

19. Hakika baada ya kugeuzwa kwangu, nalitubu; na baada ya kufundishwa kwangu, nalijipiga pajani; nalitahayarika, naam, nalifadhaika, kwa sababu naliichukua aibu ya ujana wangu.

20. Je! Efraimu siye mwanangu mpendwa? Je! Siye mtoto apendezaye? Maana kila nisemapo neno juu yake, ningali nikimkumbuka sana; kwa sababu hiyo moyo wangu unataabika kwa ajili yake; bila shaka nitamrehemu, asema BWANA.

Yer. 31