3. BWANA asema hivi, Fanyeni hukumu na haki, mkamtoe yeye aliyetekwa katika mikono ya mdhalimu; wala msiwatende mabaya mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kuwadhulumu, wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia katika mahali hapa.
4. Kwa maana mkifanya haya kweli kweli, ndipo watakapoingia kwa malango ya nyumba hii wafalme wenye kuketi katika kiti cha enzi cha Daudi, wanakwenda kwa magari, na wamepanda farasi yeye, na watumishi wake, na watu wake.
5. Lakini kama hamtaki kusikia maneno haya, mimi naapa kwa nafsi yangu, asema BWANA, ya kuwa nyumba hii itakuwa ukiwa.
6. Kwa maana BWANA asema hivi, katika habari ya nyumba ya mfalme wa Yuda;Wewe u Gileadi kwangu,na kichwa cha Lebanoni;Ila hakika nitakufanya kuwa jangwa,na miji isiyokaliwa na watu.
7. Nami nitakufanyia tayari watu wenye kuharibu,kila mtu na silaha zake;Nao watakata mierezi miteule yako,na kuitupa motoni.
8. Na mataifa mengi watapita karibu na mji huu, nao watasema kila mtu na jirani yake, Nini maana yake BWANA kuutenda hivi mji huu mkubwa?
9. Ndipo watakapojibu, Ni kwa sababu waliliacha agano la BWANA, Mungu wao, wakaabudu miungu mingine, na kuitumikia.
10. Msimlilie aliyekufa, wala msimwombolezee,Bali mlilieni huyo aendaye zake mbali;Kwa maana yeye hatarudi tena,Wala hataiona nchi aliyozaliwa.
11. Maana BWANA asema hivi, katika habari za Shalumu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; aliyemiliki badala ya Yosia, baba yake, yeye aliyetoka mahali hapa; Hatarudi huku tena;
12. bali katika mahali pale walipomchukua mateka ndipo atakapokufa, wala hataiona nchi hii tena kamwe.
13. Ole wake aijengaye nyumba yake kwa uovu!Na vyumba vyake kwa udhalimu!Atumiaye utumishi wa mwenzake bila ujira,Wala hampi mshahara wake;
14. Asemaye, Nitajijengea nyumba pana na vyumba vipana;Naye hujikatia madirisha;Na kuta zake zimefunikwa kwa mierezi,Na kupakwa rangi nyekundu.
15. Je! Utatawala kwa sababu unashindana na watu kwa mierezi? Baba yako, je! Hakula na kunywa, na kufanya hukumu na haki? Hapo ndipo alipofanikiwa.
16. Alihukumu maneno ya maskini na mhitaji; hapo ndipo alipofanikiwa. Je! Huku siko kunijua, asema BWANA?
17. Bali macho yako na moyo wako hauna utakalo ila kutamani, na kumwaga damu isiyo na hatia, na kudhulumu, na kutenda jeuri.
18. Basi, BWANA asema hivi, katika habari ya Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; Hawatamwombolezea, wakisema, Aa! Ndugu yangu; au, Aa! Dada yangu; wala hawatamlilia, wakisema, Aa! Bwana wangu; au, Aa! Utukufu wake.