Yer. 17:1-16 Swahili Union Version (SUV)

1. Dhambi ya Yuda imeandikwa kwa kalamu ya chuma, na kwa ncha ya almasi; imechorwa katika kibao cha moyo wao, na katika pembe za madhabahu zenu;

2. na wakati huo watoto wao wazikumbuka madhabahu zao, na maashera yao, karibu na miti yenye majani mabichi juu ya milima mirefu.

3. Ee mlima wangu wa uwandani, nitatoa mali zako na hazina zako zote ziwe nyara, na mahali pako palipoinuka, kwa sababu ya dhambi, katika mipaka yako yote.

4. Nawe, naam, wewe nafsi yako, utaachana na urithi wako niliokupa; nami nitakulazimisha kuwatumikia adui zako katika nchi usiyoijua; maana umewasha moto katika hasira yangu, utakaowaka milele.

5. BWANA asema hivi,Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu,Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yakeNa moyoni mwake amemwacha BWANA.

6. Maana atakuwa kama fukara nyikani,Hataona yatakapotokea mema;Bali atakaa jangwani palipo ukame,Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.

7. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA,Ambaye BWANA ni tumaini lake.

8. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji,Uenezao mizizi yake karibu na mto;Hautaona hofu wakati wa hari ujapo,Bali jani lake litakuwa bichi;Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua,Wala hautaacha kuzaa matunda.

9. Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?

10. Mimi, BWANA, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.

11. Kama kware akusanyaye makinda asiyoyazaa, ndivyo alivyo mtu ajipatiaye mali, wala si kwa haki, katikati ya siku zake zitaachana naye, na mwisho wake atakuwa mpumbavu.

12. Kiti cha enzi, cha utukufu, kilichowekwa juu tangu mwanzo, ndicho mahali patakatifu petu.

13. Ee BWANA, tumaini la Israeli, wote wakuachao watatahayarika. Wao watakaojitenga nami wataandikwa katika mchanga, kwa sababu wamemwacha BWANA, kisima cha maji yaliyo hai.

14. Uniponye, Ee BWANA, nami nitaponyeka; uniokoe, nami nitaokoka; kwa maana wewe ndiwe uliye sifa zangu.

15. Tazama, wao waniambia, Neno la BWANA liko wapi? Na lije, basi.

16. Mimi hapa sikufanya haraka kuacha kuwa mchungaji nyuma yako; wala sikuitamani siku ya maradhi ya kufisha; wewe unajua; yaliyotoka midomoni mwangu yalikuwa mbele za uso wako.

Yer. 17