1. Neno la BWANA lililomjia Sefania, mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amaria, mwana wa Hezekia; katika siku za Yosia, mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda.
2. Nitavikomesha kabisa vitu vyote, visionekane juu ya uso wa nchi, asema BWANA.
3. Nitamkomesha mwanadamu na mnyama; nitakomesha ndege wa angani, na samaki wa baharini, na hayo makwazo pamoja na wabaya; nami nitamkatilia mbali mwanadamu, asionekane juu ya uso wa nchi, asema BWANA.
4. Nami nitaunyosha mkono wangu juu ya Yuda, na juu ya watu wote wakaao Yerusalemu; nami nitayakatilia mbali mabaki ya Baali, yasionekane mahali hapa, na hilo jina la Wakemari pamoja na makuhani;
5. na wale walisujudiao jeshi la mbinguni juu ya dari za nyumba; na hao waabuduo, waapao kwa BWANA na kuapa pia kwa Malkamu;
6. na hao waliorudi nyuma, na kuacha kumfuata BWANA; na hao wasiomtafuta BWANA, wala kumwulizia.
7. Nyamaza kimya mbele za Bwana MUNGU;Kwa maana siku ya BWANA i karibu;Kwa kuwa BWANA ameweka tayari dhabihu,Amewatakasa wageni wake.
8. Na itakuwa, katika siku ile ya dhabihu ya BWANA, nitawaadhibu wakuu, na wana wa mfalme, na watu wote waliovaa mavazi ya kigeni.
9. Na katika siku ile nitawaadhibu hao wote warukao juu ya kizingiti, waijazao nyumba ya bwana wao udhalimu na udanganyifu.
10. Na katika siku ile, asema BWANA kutakuwako sauti ya kilio kutoka lango la samaki, na mlio mkuu katika mtaa wa pili, na mshindo mkuu kutoka milimani.
11. Haya! Lieni, ninyi mkaao katika Makteshi, maana wafanya biashara wote wameangamia; hao wote waliokuwa na mizigo ya fedha wamekatiliwa mbali.
12. Kisha itakuwa wakati ule, nitauchunguza Yerusalemu kwa taa; nami nitawaadhibu watu walioganda juu ya sira zao; wasemao katika mioyo yao, BWANA hatatenda mema, wala hatatenda mabaya.
13. Na huko utajiri wao utakuwa mateka, na nyumba zao zitakuwa ukiwa; naam, watajenga nyumba, lakini hawatakaa ndani yake; nao watapanda mizabibu, lakini hawatakunywa divai yake.
14. Hiyo siku ya BWANA iliyo kuu i karibu;I karibu, nayo inafanya haraka sana;Naam, sauti ya siku ya BWANA;Shujaa hulia kwa uchungu mwingi huko!