Omb. 1:13-22 Swahili Union Version (SUV)

13. Toka juu amepeleka moto mifupani mwangu,Nao umeishinda;Ametandika wavu aninase miguu,Amenirudisha nyuma;Amenifanya kuwa mtu wa pekee,Na mgonjwa mchana kutwa.

14. Kongwa la makosa yangu limefungwa na mkono wake;Hayo yameshikamana;Yamepanda juu shingoni mwangu;Amezikomesha nguvu zangu;

15. Bwana amenitia mikononi mwao,Ambao siwezi kupingamana nao.Bwana amewafanya mashujaa wangu woteKuwa si kitu kati yangu;Ameita mkutano mkuu kinyume changuIli kuwaponda vijana wangu;Bwana amemkanyaga kama shinikizoniHuyo bikira binti Yuda.

16. Mimi ninayalilia mambo hayo;Jicho langu, jicho langu linachuruzika maji;Kwa kuwa mfariji yu mbali nami,Ambaye ilimpasa kunihuisha nafsi;Watoto wangu wameachwa peke yao,Kwa sababu huyo adui ameshinda.

17. Sayuni huinyosha mikono yake;Hakuna hata mmoja wa kumfariji;BWANA ametoa amri juu ya Yakobo,Kwamba wamzungukao wawe watesi wake;Yerusalemu amekuwa kati yaoKama kitu kichafu.

18. BWANA ndiye mwenye haki;Maana nimeiasi amri yake;Sikieni, nawasihi, enyi watu wote,Mkayatazame majonzi yangu;Wasichana wangu na wavulana wanguWamechukuliwa mateka.

19. Naliwaita hao walionipendaLakini walinidanganya;Makuhani wangu na wazee wanguWalifariki mjini;Hapo walipokuwa wakitafuta chakulaili kuzihuisha nafsi zao.

20. Angalia, Ee BWANA; maana mimi ni katika dhiki;Mtima wangu umetaabika;Moyo wangu umegeuka ndani yangu;Maana nimeasi vibaya sana;Huko nje upanga hufisha watu;Nyumbani mna kama mauti.

21. Wamesikia kwamba napiga kite;Hakuna hata mmoja wa kunifariji;Adui zangu wote wamesikia habari ya mashaka yaliyonipata;Hufurahi kwa kuwa umeyafanya hayo;Utaileta siku ile uliyoitangaza,Nao watakuwa kama mimi.

22. Huo uovu wao woteNa uje mbele zako wewe;Ukawatende wao kama ulivyonitenda mimiKwa dhambi zangu zote;Kwa maana mauguzi yangu ni mengi sana,Na moyo wangu umezimia.

Omb. 1