Mwa. 28:6-14 Swahili Union Version (SUV)

6. Esau akaona ya kwamba Isaka amembariki Yakobo na kumpeleka Padan-aramu, ili ajitwalie mke huko, na katika kumbariki akamwagiza, akasema, Usitwae mke wa binti za Kanaani,

7. na ya kuwa Yakobo amewatii babaye na mamaye, akaenda Padan-aramu.

8. Esau akaona ya kuwa binti za Kanaani hawakumpendeza Isaka, baba yake.

9. Basi Esau akaenda kwa Ishmaeli akamtwaa Mahalathi, binti Ishmaeli mwana wa Ibrahimu, ndugu wa Nebayothi, kuwa mkewe pamoja na wakeze aliokuwa nao.

10. Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani.

11. Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale.

12. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake.

13. Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako.

14. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa.

Mwa. 28