Mdo 7:42-53 Swahili Union Version (SUV)

42. Basi Mungu akaghairi, akawaacha ili waliabudu jeshi la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika chuo cha manabii,Je! Mlinitolea mimi dhabihu na sadakaMiaka arobaini katika jangwa, enyi nyumba ya Israeli?

43. Nanyi mlichukua hema ya Moleki,Na nyota za mungu wenu Refani,Sanamu mlizozifanya ili kuziabudu;Nami nitawafahamisha mwende mbali kupita Babeli.

44. Ile hema ya ushahidi ilikuwa pamoja na baba zetu jangwani, kama alivyoagiza yeye aliyesema na Musa, ya kwamba aifanye sawasawa na mfano ule aliouona;

45. ambayo baba zetu, kwa kupokezana, wakaiingiza pamoja na Yoshua katika milki ya Mataifa wale, ambao Mungu aliwafukuza mbele ya baba zetu, mpaka siku za Daudi;

46. aliyepata fadhili mbele za Mungu, naye aliomba ampatie Mungu wa Yakobo maskani.

47. Lakini Sulemani alimjengea nyumba.

48. Ila Yeye aliye juu hakai katika nyumba zilizofanywa kwa mikono, kama vile asemavyo nabii,

49. Mbingu ni kiti changu cha enzi,Na nchi ni pa kuwekea miguu yangu;Ni nyumba gani mtakayonijengea? Asema Bwana,

50. Au ni mahali gani nitakapostarehe?Si mkono wangu uliofanya haya yote?

51. Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo.

52. Ni yupi katika manabii ambaye baba zenu hawakumwudhi? Nao waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki; ambaye ninyi sasa mmekuwa wasaliti wake, mkamwua;

53. ninyi mlioipokea torati kwa agizo la malaika msiishike.

Mdo 7